Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha.

JUMUIYA ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mjini Kibaha mkoani Pwani imesema Taifa linawategemea vijana katika dhana nzima itakayothibitisha wanasimamia kwa vitendo Mapinduzi katika kuondoa maovu yanayolikabili Taifa hili.

Aidha imekemea tabia ya kujigawa na kuweka makundi baina yao kwani kwa kufanya hivyo ni kudidimiza harakati na juhudi za kuimarisha jumuiya na kupambana kimaendeleo .

Mwenyekiti wa UVCCM Mji wa Kibaha, Azilongwa Bohari aliyasema hayo, mara baada ya jumuiya hiyo kufanya usafi katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Tumbi pamoja na kuchangia damu units 22 hospitalini hapo katika kuadhimisha miaka 54 ya siku ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Hata hivyo ,alisisitiza umoja na mshikamano kwa kundi la vijana.

Azilongwa alisema, serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar ,zinatakiwa kuona vijana wake wanachemchem ya maendeleo badala ya kuwa dimbwi la matatizo mitaani.

Aliwaasa vijana kwa umoja wao kujishughulisha na kuunda vikundi vya ujasiriamali ili kujiinua kimaisha .

"Tukielekea kwenye uchumi wa kati kuna kila sababu ya kupambana na umasikini,tukiwa kama vijana ,tuondokane kuwa matatizo kwenye jamii bali tuwe wapiganaji katika maendeleo na maisha yetu " alisema.

Pamoja na hayo ,Azilongwa aliwaomba wanachama na viongozi wa jumuiya hiyo kuanzia ngazi ya chini kushikamana ili kujidhatiti kwa lengo la kujenga ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Aliwataka viongozi wa chama na jumuiya kuendelea kuongeza wanachama wapya ambao ndio mtaji kwao na wapiga kura halali kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Azilongwa hakusita kusisitiza vikao vya mara kwa mara na kuwataka viongozi wa UVCCM wilayani hapo kushiriki katika vikao muhimu ili kujadili na kubuni njia mbadala za kuongeza wanachama na kuinua maendeleo ya jumuiya.

Akielezea zoezi la kuchangia damu, alishukuru wanachama waliojitokeza kuchangia na kuwezesha units 22 ambazo kwa hakika zitasaidia kuongeza mahitaji yanayotakiwa.

Alisema wamelenga kuchangia damu hospitalini hapo, kutokana na mahitaji makubwa na hospitali hiyo kupokea majeruhi wa ajali nyingi zinazotokea mara kwa mara kwenye barabara kuu ya Morogoro.
Nae katibu wa mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini,Method Mselewa,alisema mbali ya hayo wanatembelea kituo cha watoto yatima kilichopo Mkuza na kutoa misaada iliyotokana na ushirikiano wao na hisani kutoka kwa mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini ,Silvestry Koka na mkewe Selina Koka.
Mselewa alimshukuru mbunge huyo na familia yake kwa ushirikiano wao .
Baadhi ya viongozi na wanachama wa jumuiya ya vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kibaha Mjini, Pwani wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanya usafi ,na kujitolea kuchangia damu units 22, katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Tumbi ikiwa ni sehemu yao ya kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.(picha na Mwamvua Mwinyi).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...