VIJANA wajasiriamali wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wamefanikiwa kujinyanyua kiuchumi kwa kukusanya sh40 milioni, kupitia kikundi cha kuweka na kukopa (SACCOS) waliyoianzisha kwa vikundi 68 kujiunga nayo, kati ya vikundi 97 vya ujasiriamali vilivyosajiwa. 

Kati ya vikundi hivyo 68, vilivyojiunga na SACCOS, hadi sasa vikundi 12 vimepata mikopo, ambapo kila kikundi kina wanachama 30 sawa na watu 360 wameanza kunufaika kupitia sh40 milioni kwenye mikopo wanayokopeshana. 

Katibu wa UVCCM wilayani Simanjiro, Bakari Mwacha aliyasema hayo wakati akisoma taarifa ya wilaya hiyo kwa Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa wa Manyara Mosses Komba alipofanya ziara ya siku moja. Mwacha alisema kupitia SACCOS hiyo vijana hao wanachukua mikopo na kurudisha kwa wakati na uaminifu kupitia shughuli za ujasiriamali wanazozifanya. 

Alisema wanatoa ombi kwa halmashauri ya wilaya hiyo kutoa kipaumbele kwa vijana hao kuwapatia ile mikopo ya asilimia 5 ya mapato ya ndani kwani wataweza kuirejesha kwa wakati tofauti na vijana wengine. "Hawa wana uzoefu hata wakipewa mikopo inakuwa kwenye mikono salama tofauti na wengine ambao wakipewa wanasuasua kurejesha ila vijana wetu watakuwa na uhakika kwani wana SACCOS yao," alisema Mwacha 

Alisema vijana wengi wanajiunga na uanachama kwenye jumuiya hiyo ambapo hadi sasa wapo 9,205 na wengine wapya 139 wamejiunga mji mdogo wa Mirerani. Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara, Mosses Komba aliupongeza uongozi wa UVCCM wilaya ya Simanjiro, kwa kusimamia ipasavyo vikundi hivyo hadi kupatikana kwa fedha hizo na kujinufaisha kiuchumi. 

"Mmekuwa mfano bora kwa vijana wa mkoa wa Manyara, kwani wilaya nyingine zinapaswa kuiga mfano wenu wa kuchangamkia fursa za kuongeza kipato," alisema Komba. Alisema baada ya kuwa na vikundi hivyo suala la kupatiwa mikopo na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, litakuwa rahisi kwani ninyi mtakuwa na uzoefu wa kufanya ujasiriamali. 

Mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya ya Simanjiro, Thomas Mollel alisema atahakikisha anapigania upatikanaji wa asilimia tano ya mikopo kwenye halmashauri ya wilaya ili vijana wapate mikopo. Mollel alisema vijana wa Simanjiro wanapaswa kushirikiana kwa pamoja ili kujijenga kiuchumi na kujitolea nguvu kazi ili kutekeleza ilani ya CCM. 
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara Mosses Komba akipokewa na wanachama wa CCM wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro alipoanza ziara yake ya siku moja. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...