WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amegawa kadi za matibabu kwa wazee 280 wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara, kadi hizo zitawawezesha wazee hao kutibiwa bure.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa matibabu bure kwa wazee walio na umri wa kuanzia miaka 60.

Waziri Mkuu alikabidhi kadi hizo jana (Alhamisi, Januari 18, 2018) alipotembelea mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Serengeti, inayojengwa katika mji wa Mugumu.Alisema Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Serengeti itakamilisha ujenzi wa hospitali hiyo, itakayokuwa na uwezo wa kuwahudumia wakazi wa wilaya hiyo na wageni.

Waziri Mkuu alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni muhimu kwa kuwa mbali na kuwanufaisha wananchi, pia watalii wanaotembelea mbuga ya Serengeti nao wataweza kutibiwa hapo.Awali, Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Nurdin Babu alisema tangu mwaka 1974 wilaya hiyo ilipoanzishwa hadi sasa haina hospitali ya wilaya na wakazi wake wanatibiwa katika hospitali teule ya Nyerere inayomilikiwa na kanisa la Mennonite Tanzania.

Alisema kutokana na kuongeka kwa idadi ya wakazi hao pamoja na idadi kubwa ya wageni wanaotembelea Serengeti, hususan watalii hospitali hiyo haina tena uwezo wa kutoa huduma kwa kiwango kinachostahili.Bw. Babu alisema mara nyingi wageni wanaotembelea mbuga ya Serengeti hulazimika kufuata huduma za afya mjini Arusha au Nairobi nchini Kenya pale wanapougua au kupata ajali katika shughuli zao za kitalii.

Alisema kwa upande wa wakazi wa wilaya ya Serengeti wao hulazimika kufuata huduma za afya katika hospitali ya Mkoa au hospitali ya Rufaa ya Bugando, hivyo kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa hospitali utawapunguzia kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Pia Mkuu huyo wa wilaya alisema alianzisha kampeni ya changia sh. 1,000 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya, kwa lengo la kuwafanya wakazi hao wajisikie kuwa wameshiriki katika ujenzi huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, JANUARI 19, 2018.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi kadi ya matibabu ya bure kwa wazee, Johaness Chacha, moja wa wazee 280waliopatiwa vitambulishbo hivyo vitakavyowawezesha kutibiwa bure popote wilayani Serengeti katika makabidhiano yaliyofanyika kwenye viwanja vya hospitali ya wilaya ya Mugumu Januari 18, 2018. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...