Na Greyson Mwase, Chato
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani  leo  tarehe 13 Februari, 2018 amefanya ziara katika wilaya ya Chato mkoani Geita lengo likiwa ni kukagua miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na  Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Akizungumza kwa nyakati tofauti  na wananchi katika vijiji vya Iparamasa na Kalembela vilivyopo wilayani Chato mkoani Geita, Dkt. Kalemani ameitaka kampuni iliyopewa kazi ya kujenga miundombinu ya umeme katika vijiji husika, ya White City JV Guandong kukamilisha kazi  iliyopewa ndani ya  wiki moja  katika kijiji cha Iparamasa na  siku tatu katika kijiji cha Ilembela ili wananchi waanze kunufaika na huduma ya umeme wa uhakika.
“ Wananchi hawa wamechoka na adha ya kukosa  huduma ya umeme kwa muda mrefu, ninatoa wiki moja kwa mkandarasi kuhakikisa kijiji cha  Iparamasa kinapata umeme wa uhakika na siku tatu kwa kijiji cha Kalembela wanapatiwa huduma ya umeme kwa kuwa tayari nguzo zimefika katika vijiji husika,” alisema Dkt. Kalemani
Waziri Kalemani aliendelea kusema kuwa Serikali kupitia  Wizara ya Nishati, imepanga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia ya 75 ya watanzania wanapata huduma ya umeme ambao ni wa uhakika na kuchangia nchi kutoka kwenye orodha ya nchi masikini na kuingia kwenye orodha ya nchi za kipato cha kati
Alisisitiza kuwa, kwa kutambua mchango wa nishati kwa ukuaji wa uchumi wa viwanda, Wizara ya Nishati imepanga mikakati ya kuhakikisha miradi ya REA inatekelezwa kwa wakati kwa kutenga fedha za kutosha, na usimamizi  makini ili wananchi wote wanufaike na huduma ya umeme.
Aidha, katika hatua nyingine Dkt. Kalemani aliwataka wananchi  wa vijiji husika kujiandaa na huduma ya umeme kwa kutandaza nyaya kwenye nyumba zao (wiring) au kuweka  Kifaa Maalum cha Umeme Tayari (UMETA) ili waunganishwe na huduma ya umeme  mapema.
Pia  Waziri Kalemani aliwataka wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza mara baada ya upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika kama vile uanzishwaji wa viwanda vya kusindika nafaka, mashine za kuchomea vyuma na kuondokana na umaskini.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akielezea matumizi ya Kifaa Maalum cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa kijiji cha Iparamasa (hawapo pichani) wilayani Chato mkoani Geita.
 Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kalembela kilichopo wilayani Chato mkoani Geita, wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kalembela kilichopo wilayani Chato mkoani Geita.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa mkandarasi, wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika  kijiji cha Kalembela kilichopo wilayani Chato mkoani Geita.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akisalimiana na mmoja wa wananchi mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kalembela kilichopo wilayani Chato mkoani Geita.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...