Duniani kote, vifo vya watoto wachanga bado viko juu sana kiasi cha kuwa tishio, hasa miongoni mwa nchi maskini zaidi ulimwenguni, UNICEF imesema katika ripoti yake mpya kuhusu vifo vya watoto iliyozinduliwa leo mjini New York. Ripoti hiyo imebainisha kuwa watoto wanaozaliwa katika nchi za Japani, Iceland na Singapore wana nafasi kubwa zaidi ya kuishi, wakati wale wanaozaliwa katika nchi za Pakistani, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Afghanistani wanakabiliana na hatma mbaya kabisa ya maisha yao.

 “Wakati ambapo tumepunguza kwa zaidi ya nusu idadi ya vifo miongoni mwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano katika robo karne iliyopita, bado hatujafaulu kwa kiwango kama hicho katika kukomesha vifo miongoni mwa watoto walio na umri wa chini ya mwezi mmoja,” alisema Henrietta H. Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF. 

“Kwa kuwa vifo hivi vingi vinazuilika, ni wazi kwamba, tumewaangusha watoto walio maskini zaidi duniani,” alisisitiza mkurugenzi huyo wa UNICEF. Ulimwenguni, katika nchi za kipato cha chini, wastani wa vifo vya watoto wachanga ni vifo 27 katika kila vizazi hai 1,000, ripoti inasema. Katika nchi za kipato cha juu, kiwango ni vifo 3 kwa kila vizazi hai 1,000. Nchini Tanzania, viwango vya vifo vya watoto wachanga ni 25 katika kila vizazi hai 1,000, kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya wa Tanzania (TDHS 2015-16). 

Ikiwa kila nchi itapunguza viwango vya vifo vya watoto wake wachanga hadi katika viwango vya nchi za kipato cha juu ifikapo mwaka 2030, maisha ya watoto milioni 16 yataokolewa, ripoti hiyo imebainisha. Ripoti hiyo inaeleza pia kwamba miongoni mwa maeneo 8 kati ya 10 yaliyo hatari zaidi kwa mtu kuzaliwa, basi Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, ni mojawapo, ambapo wanawake wajawazito wana uwezekano mdogo wa kupata msaada wakati wa kujifungua kwa sababu ya umaskini, migogoro na taasisi zisizo na ufanisi. Watoto wanaozaliwa katika nchi zenye hatari zaidi wana uwezekano wa hadi mara 50 wa kufa kulinganisha na wale wanaozaliwa katika nchi zilizo salama. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...