Rais wa Jamhuri ya Muungano wa 
 Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli 

 Tangu Jumapili tarehe 11/02/2018 nilishtushwa na habari iliyoandikwa na mwandishi aitwaye David Ng’ang’a kupitia mtandao uitwao “Business Insider” ikiwa na kichwa cha habari kisemacho “Marry two or more women to reduce prostitution among ladies – Magufuli to Tanzanian men” ikiwa na maana Rais Magufuli amewaambia wanaume wa Tanzania waoe wake wawili au zaidi ili kupunguza umalaya kwa wanawake. 
 Kwanza habari yenyewe imejaa uongo na uzandiki wa hali ya juu. Ina takwimu za uongo kuwa Tanzania ina wanawake milioni 40 na wanaume milioni 30, yaani jumla Tanzania ina watu milioni 70??
Uongo na upuuzi mkubwa, kwamba Rais Magufuli alikuwa akizungumza na wanaume 14,000 waliokuwa mafunzoni? Uongo wa kupigiwa mfano, kwamba wanawake wa Tanzania wanalia kukosa wanaume?? Uongo na udhalilishaji wa hali ya juu, kwamba serikali itatoa ruzuku kwa wanaume watakaooa wanawake wawili au zaidi?? 
Uongo na uchochezi wa hali ya juu, na kwamba Tanzania ina viwango vya juu vya umalaya Afrika Mashariki?? Uongo na udhalilishaji usiovumilika. 
 Nilishtushwa kwa sababu kauli hizi haziwezi kutamkwa na kiongozi tena kiongozi mwenyewe akiwa ni Rais Magufuli ambaye ameaminiwa na Watanzania na anayetosha kwa sifa za kiongozi makini, asiye na ubaguzi, mwenye upendo, mpigania wanyonge na mwenye maono ya kuifikisha Tanzania katika neema. 
Sijawahi kumsikia mahali popote Rais Magufuli akitamka maneno hayo na kwa utamaduni wa kitanzania na viongozi watokanao na Chama Cha Mapinduzi hizi sio kauli za kiungwana. Nilipofuatilia nikabaini kuwa mwandishi wa makala hii ni wa nchi jirani, nilipofuatilia zaidi nikabaini kuwa makala hii inachochewa na kushabikiwa na wanasiasa za upinzani nchini Tanzania. Kwa kifupi nikabaini kuwa hapa kuna mbinu za kumchafua Rais Magufuli kutoka nchi jirani na pia wanasiasa wanataka kupata maslahi ya kisiasa kwa kupambisha upuuzi huu. 
 Nimeona niandike kumjulisha aliyepika uongo huu kuwa takataka alizoandika hazina maana yoyote na kamwe hazitarudisha nyuma juhudi za Rais Magufuli na Watanzania kujenga nchi yao. 
 Nimeona nimjulishe kuwa Watanzania wanamjua Rais wao na dunia inajua kuwa Tanzania kuna Rais Magufuli wa mfano kwa Marais wote wa Afrika, kuna Rais Magufuli ambaye ameamua kwa dhati kupigana na rushwa na anafanikiwa sana, kuna Rais Magufuli ambaye amesema hakuna atakayeendelea kuinyonya Tanzania, kuna Rais Magufuli ambaye hakubaliani na danganya toto iliyosababisha Tanzania kuwa shamba la bibi, kuna Rais Magufuli ambaye ameanza kutekeleza miradi mikubwa, anakuza uchumi na anasimamia utendaji kazi katika ofisi za umma na hataki mchezo dhidi ya vitendo vyote vya kuirudisha nyuma Tanzania na kuwanyanyasa Watanzania hasa wanyonge. 
 Nimejua kuwa kinachowasumbua wengi ni mwangwi wa mafanikio ya muda mfupi aliyoyapata Rais Magufuli katika miaka miwili ya tangu Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Na hiki ni kipimo cha kuwajua wanaoitakia mema Tanzania, na kwa namna yoyote wasioitakia mema Tanzania lazima wataponda kazi zinazofanywa na Rais makini Dk. Magufuli. 
 Wapo walioumizwa na kuanza kujengwa kwa reli ya kati (Standard Gauge) kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na baadaye kuendelea hadi Dodoma na Isaka, wamekasirika zaidi waliposikia taarifa za ghafla kuwa Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame amekubaliana na Rais Magufuli kuunganisha reli ya Standard Gauge kutoka Isaka hadi Kigali nchini Rwanda. 
Wanajua kuwa sasa bandari zao zinakwenda kukosa mizigo ya Rwanda. Kabla yake waliumizwa na makubaliano ya Rais Magufuli na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuhusu kuunganisha reli ya kati hadi Kampala ili mizigo yote ya Uganda itumie bandari ya Dar es Salaam. 
 Pia wameumizwa baada ya kuona Tanzania imeshinda mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Rwanda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, wanajua kuwa sasa mabilioni ya dola za mradi huu mkubwa yatatua Tanzania na Watanzania lukuki watapata ajira na kuongeza vipato. 
 Wamekasirika zaidi kusikia habari za Tanzania kuanza kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha megawatts 2,100 katika mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), wanajua kuwa matarajio yao ya kuuza umeme Tanzania yamepotea, wanajua kuwa upepo wa wawekezaji ambao walishindwa kuja Tanzania na kwenda nchi mwao sasa utabadili mwelekeo na kuvumia Tanzania. 
 Wamechukia kwamba kwa hatua ambazo Tanzania inazichukua kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kuondoa urasimu katika uwekezaji, kupambana na rushwa na kuusimamia vizuri uchumi kutaifanya Tanzania kuwa nchi itakayoongeza kasi isiyoshikika ya ukuaji wa uchumi ambao hata sasa inaongoza kwa Afrika Mashariki kwa ukuaji wa asilimia 6.8, na kuwa ya nchi tatu kwa ukuaji barani Afrika. 
 Wamenuna sana kuona utekelezaji wa azma ya ujenzi wa viwanda ukienda kwa kasi kubwa, imewaudhi sana kusikia ndani ya miaka miwili viwanda 3,500 vimejengwa na sasa Tanzania inazungumza kununua bidhaa za ndani kwa wananchi wake. 
 Hawana amani kabisa wanaposikia Rais Magufuli na Serikali yake wameanza kufufua shirika la ndege la Taifa (ATCL) kwa kununua ndege sita ikiwemo ndege kubwa yenye uwezo wa kuruka moja kwa moja hadi Ulaya, China na Marekani, na ndege nyingine zitakazoruka ndani ya bara la Afrika na hivyo kukuza uchumi kupitia utalii na biashara. Wanajua kuwa hii ina madhara makubwa kwenye uchumi wao. 
 Hawapendi kabisa kuona washirika wa maendeleo wanazidi kuongeza imani na kuongeza fedha katika miradi mbalimbali ya kujenga uchumi na kuhudumia wananchi. 
Walitarajia kuona baada ya Rais Magufuli kuchukua hatua alizochukua pengine wadau wa maendeleo wangesusia lakini ndio kwanza Benki ya Dunia imeongeza pesa, Benki ya Maendeleo Afrika imeongeza pesa, achilia mbali nchi mbalimbali ambazo zinatoa misaada kila uchao zikiwemo China, Marekani, Uingereza, nchi za Uarabuni na nyinginezo nyingi. 
 Unaweza kusema mengine lakini hali ndio hii, na hata wale waliokuwa wanabeza na kujiona wao ni bora, sasa wanaumbuka kutokana na mambo kuwaendea kombo. Hizi ni salamu nzito sana. Na kwa wanasiasa wa ndani ya Tanzania nawakumbusha msemo maarufu “kama huwezi kushindana nae, ungana nae” cha ajabu madiwani wengi wamelijua hili mapema na wanazidi kumiminika kuhama kutoka siasa za upinzani na kujiunga na chama tawala, hapa somo ni moja tu wamegundua kama kweli kiongozi ana nia ya kuwapigania wananchi dawa ni kuungana na Rais Magufuli kupigania watu wake. 
 Wameshtuka kuwa yale ambayo Rais Magufuli na Serikali wanayasimamia ndio yale ambayo vyama vyao vya siasa viliyahubiri kwa miaka mingi na sasa vyama hivyo havitaki tena kuyasema na kuyapigania na badala yake waliotuhumiwa kuiangamiza nchi na kuwaumiza wananchi wamekaribishwa kwenye vyama vya upinzani na wamekaa meza za mbele (hightable). 
 Hivi sasa imekuwa ndio siasa za upinzani kwa viongozi wake kupinga kila anachokifanya Rais, wamegawana majukumu ya kumdhohofisha bila mafanikio. Ukigeukia huku utamkuta Freeman Mbowe anamshambulia Rais, ukigeuka kule utamkuta mgonjwa Tundu Lissu anaacha kushughulika na matibabu yake anamshambulia Rais, Zitto Kabwe kasahau hata chama chake cha ACT kinachopukutika amejipa kazi ya kumshambulia Rais, Julius Mtatiro amekuwa mwanamitandao maarufu wa kumshambulia Rais na Mawaziri. 
 Kazi ni hiyo hiyo kwa wengine ambao Watanzania wamewapuuza akina Godbless Lema, Mchungaji Peter Msigwa, Halima Mdee, Ester Bulaya na wabunge wengine wa chama cha CHADEMA na viongozi wao wa chama. Napata wasiwasi kuwa upinzani Tanzania umeishiwa mbinu za kufanya siasa na sasa unatukana tu, unashambulia personalities za viongozi na kupika taarifa ili kuleta taharuki. 
Wengine wanachokoza vyombo vya dola ili wapate umaarufu wa kukamatwa na kulalamika kuwa wanaonewa. Hata hawashtuki kwa nini wanayemshambulia hawajibu? Hawajiulizi Watanzania wanawaonaje? Hawajiulizi kwa haya wanayofanya ikitokea siku wao wakashika nchi watafanya hayahaya ama itawalazimu kubadilika na kuwapa Watanzania haya anayowapa Rais Magufuli. 
 Kwa ninavyomjua Rais Magufuli, wanachofanya nchi jirani na wanasiasa za upinzani Tanzania ni patapotea, na kizuri ni kwamba Watanzania wanaelewa na wanakwenda kwa mwendo wa Rais Magufuli. 

 Naamini wamesoma andiko hili na ujumbe umefika 
 Alamsiki 
 Fabian Mdondolelo 
 13 Februari, 2018 
 Dar es Salaam

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...