Watoto sita ambao wamewekewa vifaa vya usikivu Januari mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wameanza kusikia kwa mara ya kwanza baada ya kuwashiwa vifaa hivyo.

Kuwashwa kwa vifaa hivyo kumeleta furaha kwa wazazi kwani wameshuhudia watoto wao wakisikia sauti kwa mara ya kwanza na hivyo kuwajengea matumaini ya watoto hao kuanza maisha mapya.

Zoezi la kuwawashia vifaa hivyo (Switch On) limefanyika leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na wataalaam kutoka Medel Austria ambao ndio wasambazaji wa vifaa hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari , Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio Dkt. Edwin Liyombo amesema watoto hao walifanyiwa upasuaji wa upandikizaji kifaa cha usikivu Januari mwaka huu ambapo zaidi ya asilimia 80 ya upasuaji huo ulifanywa na watalaam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili .

‘’Watoto hawa wataanza maisha mapya ya kusikia sauti mbalimbali katika mazingira yanayowazunguka baada ya kuunganisha vifaa hivi na kuviwasha’’. Amesema Dkt. Liyombo

Akifafanua amesema mbali na watoto hao sita lakini pia watoto wengine watano ambao walifanyiwa upasuaji huo mwaka jana na wengine sita ambao walifanyiwa upasuaji huo nchini India nao wamekuja kufuatiliwa maendeleo yao ili kubaini changamoto zinazowakabili na kupewa ushauri wa kitaalam. 

Akielezea ukubwa tatizo Dkt. Liyombo amesema takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonesha kuwa katika watoto 1,000 wanaozaliwa, inakadiriwa kuwa watoto watano wanazaliwa na tatizo kubwa la usikivu .

Pia amesema MNH ipo kwenye mchakato wa kuanzisha utaratibu wa kuwachunguza watoto wachanga ili kubaini mapema wenye matatizo yakutosikia.

Kwa upande wake Muwakilishi kutoka Medel Fayaz Jafar amesema upasuji huo umekua na mafanikio makubwa kwakua katika awamu hiyo kumekua na mabadiliko kwani asilimia kubwa ya upasuaji umefanywa na watalaam wa MNH na kwamba hatua hiyo ni ya kuridhisha.

Huduma ya Upandikizaji wa kifaa cha usikivu (Cochlear Implant) ilizinduliwa Juni 7 , 2017 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto Mheshimiwa Ummy Mwalimu hivyo Tanzania imekuwa nchi ya pili kutoa huduma hiyo katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki baada ya Kenya. Aidha Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hiyo kupitia Hospitali ya Umma ambayo ni Muhimbili yenye hadhi ya ubingwa wa hali ya juu.
Mtaalam wa Huduma ya Usikivu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Mathayo Majogoro Alfred (katikati) akiunganisha kifaa cha usikivu cha nje na cha ndani ili mtoto Matilda Katobesi aweze kusikia kwa mara ya kwanza. Kulia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio, Dkt. Edwin Liyombo akifuatilia na kushoto ni mama wa mtoto huyo, Angelina Cosmas.
Mtoto Matilda kwa mara ya kwanza leo tarehe 24, Januari, 2018 akianza kutamka baadhi ya maneno baada ya kufundishwa na mtaalamu wa sauti kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Pua, Koo na Masikio, Dkt. Edwin Liyombo wa Muhimbili akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuwasha kwa mara ya kwanza vifaa vya usikivu kwa watoto waliofanyiwa upasuaji na kupandikizwa vifaa hivyo katika hospitaili hiyo. Kuanzia kushoto ni Mkuu wa Idara ya Macho, Dkt. Baruani, Katibu wa Umoja wa Watoto na Wazazi Wanaonufaika na Vifaa vya Usikivu nchini, Bupe Mwakalambile na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja, Bwana Aminiel Aligaesha.
Wazazi wakisubiri kuashwa kwa mara ya kwanza kwa vifaa vya usikivu katika hospitali hiyo.
Mtaalamu wa Sauti, Fayaz Jaffer akionyesha kifaa cha usikivu (Cochlear Implant) kwa waandishi wa habari ambacho kinapandikizwa kwa mtoto mwenye tatizo la kusikia. Kulia ni Paul Khalil kutoka Kampuni ya Medel. Kuanzia kushoto ni Dkt. Edwin Liyombo, Dkt. Baruani, Bi. Bupe Mwakalambile na Bwana Aminiel Aligaesha wakiwa kwenye mkutano huo leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...