Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli leo ameongoza maelfu ya wanawake wa mkoa wa Dar es salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani huku akiziomba asasi za kiraia, na watu binafsi kushirikiana na serikali kuwapatia kinamama mbinu mbalimbali, mafunzo, mitaji na kuwatafutia masoko ya bidhaa zao.
Mama Magufuli pia ameupongeza mkoa wa Dar es salaam kwa kuanzisha vikundi zaidi ya 400 vya wanawake vinavyojishughulisha na shughuli mbali mbali ikiwemo usindikaji mazao, ushonaji, uchoraji na kadhalika, pamoja na kuwa na vikundi vya kukopeshana (VICOBA) vipatavyo 2,748 ambavyo kwa pamoja vina mtaji wa jumla ya shilingi bilioni 10.78.
"Ni imani yangu kuwa kama mikoa yote na taasisi nyingine za kiserikali na kiraia zitaiga mfano wa Dar es salaam katika kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuwashirikisha kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda basi tutawawezesha wanawake kiuchumi ikiwemo kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda", alisema Mama Magufuli amesema kwenye sherehe hizo zilizofanyika ukumbi wa Mlimani City.
Huku akishangiliwa kwa nguvu, Mama Magufuli amesema japokuwa serikali inajitahidi sana kuweka usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake kisiasa, kiuchumi, elimu na afya, serikali peke yake haiwezi kuzimaliza changamoto zote, hivyo ni lazima wananchi wenyewe washiriki katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Mama Magufuli amewapongeza viongozi wa awamu zote za nchi, ikiwa ni pamoja na kinamama shupavu wa TANU na ASP na baadaye CCM ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika harakati za kumkomboa mwanamke nchini.
"Kutokana na umuhimu wa siku ya leo naomba nitambue mchango wa Mama Maria Nyerere, Mama Fatma Karume, Bibi Titi Mohamed, Mama Sophia Kawawa, Bi. Hadija Jabir, Bi Johari Yusuf Akida, Mwajuma Koja, Bi. Mtumwa Fikirini na wengineo wengi. Hatuna budi kuwapongeza sana akinamama hawa kwa kupigania haki za wanawake nchini" alisema.
Mama Magufuli ametanabahisha kwamba japokuwa vitendo vya unyanyasaji, dhuluma na ukatili dhidi ya wanawake bado vinaendelea kwenye baadhi ya maeneo nchini, Tanzania  imepiga hatua kubwa na ni  miongoni mwa nchi zinazosifika duniani kwa kulinda na kusimamia haki na maslahi ya wanawake.
"Hivyo basi hatuna budi kuwapongeza wote walioshiriki katika kulinda na kutetea haki na maslahi ya wanawake nchini", alisema, kabla ya kutembelea maonesho ya wajasiriamali kinamama waliopanga bidhaa zao katika kila pembe ya ukumbi huo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda pamoja na wakuu wa Wilaya za Kinodnoni na Ilala, Mhe. Kisare Makori na Bi. Sophia Mjema. 
Wengine ni Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Dar es salaam Mama Kate Kamba, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Naibu Kamishna wa Magereza Tusekile Mwaisabila pamoja na maafisa  watendaji wa wilaya ya Ubungo.
 Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akijumuika na  maelfu ya wanawake wa mkoa wa Dar es salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam leo Machi 8, 2018
 Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akijumuika na kwaya ya wanawake wa mkoa wa Dar es salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam leo Machi 8, 2018  

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akijumuika kucheza na kuimba nyimbo za hamasa na wanawake wa mkoa wa Dar es salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam leo Machi 8, 2018  
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda akiongea machache kabla ya kumkaribisha  Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli kuhutubia  wanawake wa mkoa wa Dar es salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam leo Machi 8, 2018  
  Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akihutubua maelfu ya wanawake wa mkoa wa Dar es salaam wakati wa kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam leo Machi 8, 2018
Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akitembelea maonesho ya bidhaa mbalimbali za wajasiriamali  wanawake wa mkoa wa Dar es salaam wakati wa kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam leo Machi 8, 2018. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...