MWANAFUNZI wa Shahada ya Sheria mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Amaniel Furahini(21) ameiomba serikali na watanzania kumsaidia kulipa ada ili aweze kuendelea na masomo yake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Mwanafunzi huyo amesema amekuwa akisoma katika mazingira magumu kutokana na kukosa ada huku akidai kuwa wazazi wake hawana uwezo wa kumsomesha kwa kuwa ni wakulima wanaotegemea mvua za msimu wilayani Same.

Amesema alipochaguliwa kujiunga na masomo kwa mwaka 2017/18, aliomba mkopo kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HELB) ambao alitegemea ungeweza kuwa msaada mkubwa lakini hakuweza kufanikiwa kupata.

Furahini amesema kutokana na hali hiyo aliweza kuhangaika na kufanikiwa kulipa ada kiasi cha Sh.350,000 kati ya Sh. Milioni 1.5 anazotakiwa kulipa kwa mwaka chuoni hapo.“Hizi fedha nilizipata kutokana na kazi ya kubeba mizigo ya Watalii waliokuwa wakipanda Mlima Kilimanjaro na Meru ambapo pia nilifanikiwa kulipa fedha ya ‘Accommodation’ kiasi cha Sh.186,000 kwa muhula wa kwanza ambao umeisha,”amesema Mwanafunzi huyo.

Furahini amesema alishawasilisha suala lake kwenye uongozi wa Chuo na kwamba alishauriwa alipe kidogo kidogo au arudi nyumbani jambo ambalo anadai kuwa kwake ni vigumu kwa kuwa hana kitu chochote kinachomuingizia kipato na wazazi wake hawana uwezo.

“Nadaiwa fedha nyingi na wazazi wangu nimewaambia kwa kuwa hawana uwezo wamesema nirudi tu, na mimi nahitaji kusoma ili nifikie ndoto zangu, naiomba serikali, watanzania na wafadhili mbalimbali wanisaidie nifikie ndoto zangu maana hadi ikifika Julai mwaka huu kama nitakuwa sijalipa nitafukuzwa chuo,”ameomba Mwanafunzi huyo.

Akizungumzia maisha yake chuoni, Mwanafunzi huyo amesema amekuwa akisaidiwa na ndugu, jamaa na marafiki ambao ni wanafunzi wenzake.

“Wamekuwa wakinisaidia kuninunulia chakula naishi kwa misaada ya rafiki zangu chuoni, sasa kwenye suala la ada ndo limekuwa gumu kwangu nimekosa msaada.Naomba msaada wa kusomeshwa kwa watanzania watakaoguswa na ombi langu,”amesema Furahini.Amesema amemaliza kidato cha sita mwaka 2017 katika Shule ya Sekondari Kalangalala ambayo ipo mkoani Geita na alifanikiwa kupata ufaulu daraja la kwanza uliomuwezesha kujiunga na chuo hicho.

Furahini amesema anaona kama ndoto zake za kuisaidia nchi yake zikizimika kama asipoweza kulipa ada ili aendelee na masomo yake.

NAMBA YAKE YA MAWASILIANO - 0678873841

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...