Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.


*Mambosasa asema watamchukulia hatua za kisheria, atoa onyo kali

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
KAMANDA wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Abdul Nondo(24), aliyedai kutekwa  na watu wasiojulikna siku za karibuni uchunguzi wao umebaini kumbe alikwenda kwa mpenzi wake mkoani Iringa.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Mambosasa amefafanua Machi 6 mwaka huu ,kuanzia saa sita usiku zilianza kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mwanafunzi huyo ametekwa na watu wasiojulikana na kusababisha hofu kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla.

Kamanda Mambosasa amesema kutokana na taarifa hizo, Polisi walianza kufuatilia ili kubaini ukweli wake ikiwa pamoja na kufungua jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSM/KIN/CID/P.E/51/2018.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Machi 7 mwaka huu tulipata taarifa kutoka kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, mwanafunzi huyo ameonekana mkoani Iringa katika Wilaya ya Mafinga akiwa mwenye afya njema.

"Tena anajitambua  na akiendelea na shughuli zake na wala hakuna mahali popote ambapo ametoa taarifa kwenye kituo cha Polisi kuwa amtekwa.Jeshi letu la Polisi kwa kushirikiana na wenzetu wa Iringa tulifanya uchunguzi na kubaini  Nondo hakutekwa bali alijiteka kwa lengo la kutafuta umaarufu kwa jamii,"amesema Mambosasa.

Ameongeza baada ya kuendelea na uchunguzi wao kutokana na taarifa za tukio hilo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam wamebaini mwanafunzi huyo aliyedai alitekwa kumbe alikwenda kwa mpenzi wake."Wakati tunafuatilia tukabaini mawasiliano kati yake na huyo mpenzi wake ya mara kwa mara wakati akiwa njiani akielekea Iringa,"amesema Mambosasa.

Amefafanua Polisi pamoja na kuchunguza mambo mbalimbali kuhusu mwanafunzi huyo walitumia utaalamu wao kufuatilia mawasiliano yake kwa kipindi ambacho anadai alikuwa ametekwa lakini walichoona alikuwa anawasiliana zaidi na mpenzi wake.

Pia amesema hata baada ya mwanafunzi kupelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa alipimwa na kubaini hakuna aina yoyote ya kinywaji ambacho alipewa wala hakuwa amepewa dawa za usingizi."Hakuna na majeraha ya aina yoyote kwenye mwili wake,"amesisitiza Mambosasa na kuongeza "Uchunguzi umebaini alikuwa kwa mpenzi wake na alimua kutoa taarifa hizo kwa lengo la kujitafutia umaarufu kwa umma".

Kutokana na mazingira hayo Mambosasa amesema kwa kuwa mwanafunzi huyo hakuwa ametekwa watamchukulia hatua za kisheria kama wahalifu wengine huku akitoa onyo kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam halitavumilia mtu anayejitafutia umaarufu kwa njia ya aina hiyo na nyingine zinazofanana na hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...