Na Mwandishi Maalum
Jumla wa wagonjwa wa akili 55 waliokuwa  wametenda makosa mbalimbali yakiwamo ya jinai wakiwa na  ugonjwa wa akili, wameachiwa huru baada ya mahakama kutowatia hatiani.
Hayo yameelezwa leo  mjini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi ( Mb) wakati alipokuwa akiwasilisha  Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara Katiba na Sheria na Taasisi zake kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.  Kamati hiyo ilikuwa nchini ya Uenyekiti wa Mhe. Najma Murtaza Gingo ( Mb). Waziri  Kabudi ameieleza  Kamati hiyo kwamba,   kifungu cha 219 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20, kinampatia Waziri mwenye dhamana ya masuala ya  sheria mamlaka ya kuwaachia huru wagonjwa wa akili waliotenda makosa mbalimbali ya jinai yakiwamo ya mauaji.
“ Kutokana na mamlaka hayo ya kisheria,  katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, nilisaini hati ya kuachiliwa huru wagonjwa 55 wa akili waliotenda makosa mbalimbali ya jinai wakiwa na ugonjwa wa akili na hivyo mahakama  kutowatia hatiani” akabainisha Waziri Kabudi.
Na kuongeza kwamba, kwa muda mrefu wagonjwa hao walikuwa wakihifadhiwa kwenye Taasisi ya Isanga kusubiri amri ya Waziri. "Na kutokana  na hali ya afya zao za akili kuimarika, niliamua waachiliwe huru, ili waungane na familia zao na kuendelea na matibabu wakiwa nje ya taasisi hiyo”.
Pamoja na kuelezea kuachiwa huru kwa wagonjwa wa  akili, Waziri Kabudi pia alianisha mafanikio mbalimbali yaliyotekelezwa na Wizara pamoja na  Taasisi zake katika suala zima la utoaji na usimamiaji wa haki katika kipindi cha bajeti cha 2017/2018.Baadhi ya  mafanikio hayo ni  kwa Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  katika uendeshaji wa mashauri ya daawa ili pata ushindi katika mashauri 82 yaliyokuwa na thamani ya shilingi 1,064,581,955,743bn/-. Kwa mujibu wa  Waziri wa Katiba na Sheria  ushindi huo umewezesha pamoja na mambo mengine maamuzi ya serikali pamoja na sheria za nchi kutobadilishwa kwa msingi ya kuikuka Katiba.
Mafanikio  mengine ambayo yametajwa na   Waziri Kabudi ni pamoja na Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea na utoaji wa ushauri wa kisheria kwenye mikataba na makubaliano mbalimbali  yanayofanywa na Wizara Idara na Taasisi za Serikali. Katika eneo hilo , hadi kufikia mwezi  February, 2018 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilifanya uhakiki  na kutoa ushauri wa mikataba 691 yenye thamani ya Shilingi 1,720,026,713,823bn/- na Dola za Kimarekani 1,0884,472,366, mikataba hii ilihusu ununuzi , ukarabati wa majengo, utoaji wa huduma za jamii na ujenzi wa barabara.
Katika uendeshaji wa kesi za jinai,  Waziri wa Katiba na Sheria alieleza Kamati ya kudumu ya   Bunge ya Katiba na Sheria kwamba, katika kipindi kinachoishia February 2018. Ofisi ya  Taifa ya Mashtaka iliendelea na kuratibu shughuli za upelelezi wa makosa ya jinai mahakamani.Mashauri ya jinai yaliyoshughulikiwa ni pamoja na yaliyohusu wanyamapori, dawa za kulevya, uhujumu uchumi, rushwa  na mauaji. Ambapo washtakiwa waliotiwa hatiani walipewa adhabu mbalimbali zikiwamo vifungo, faini na mali kutaifishwa ambapo jumla ya shilingi za kitanzania 2,169 ,983,500 zilitozwa kama faini kutoka kwa washtakiwa.
Aidha kwa upande wa mali zilizotaifishwa ni pamoja na  kilogramu 24.5 za dhahabu yenye thamani ya Shilingi 2,012,357,164 na fedha za kigeni kutoka  mataifa 15 zenye thamani ya shilingi 908,019,979. Mali nyingine zilizotaifishwa ni pamoja na  magari matano ya kifahari aina ya Range Rover Vogue na moja aina ya Audi yaliyokamatwa katika banari ya Dare s Salaam yakisafirishwa kama nguo za mitumba.
Mali nyingine   zilizotaifishwa katika  kipindi hicho ni pikipiki, mifugo, mafuta na  basi la abiria lililokuwa likitumika kusaifirishia meno ya tembo  yanazokadiriwa kuwa na thamani ya jumla ya shilingi 3,242,787, 915.
Kwa upande wa  uandishi wa Sheria, Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, iliandaa jumla ya miswaada 15 ya sheria ambayo iliwasilishwa Bungeni na kupitishwa na kuwa sheria. Hali kadharika, iliadaa sheria ndogo na matamko mbalimbali ya serikali yapatayo 164 ambayo yalichapishwa kwenye gazeti  la serikali.
Mpango  na Makadirio ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2018/2019,   Wizara inaomba takribani Shilingi 183,223,038,000bn/- zikiwamo fedha za mishahara,  matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo.
Katika kikao cha leo  mafungu yaliyopitishwa  na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Sheria na Katiba   ni yale ya Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka .  
Kikao hicho  cha uwasilishaji wa   mpango na bajeti ya Wizara kilihudhuriwa pia na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi,  Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchome , Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Paul Ngwembe, Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Bw. Biswalo Mganga, pamoja na wawakilishi kutoka  Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Taasisi ambazo zipo chini ya  Wizara ya Katiba na Sheria ni Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala  Bora, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo na Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto.
 Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe Profesa Palamagamba Kabudi ( Mb) akiwasilisha  mbele ya  wajumbe wa Kamati ya  Bunge ya Kudumu ya Katiba na Sheria Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara na Taasisi zake leo  Dodoma, pembeni yake ni  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk.Adelardus Kilangi
 Mbunge wa Ubungo Mhe. Saeed Kubena ambayi ni mjumbe  wa  Kamati ya Kudumu ya  Bunge  ya Katiba na Sheria  akinyosha mkono  kuashiria kutaka kuuuliza jambo wakati  mara baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi kuwasilisha  Mpango na Makadirio ya Bajeti.
 Sehemu ya  wajumbe wa  Kamati ya  Bunge ya Kudumu ya Katiba na Sheria  wakisikiliza uwasilishwaji wa Mpango na   Makadirio ya  Bajeti ya Wizara  ya Katiba na Sheria na Taasisi zake leo mkoani  Dodoma

Naibu  Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu  ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Gingo (kushoto) akiteta jambo na Katibu wake  wakati wa uwasilishaji wa Mpango na Makadirio ya  Bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...