Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameondoka nchini jana kwenda London, Uingereza kushiriki kwenye Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 20 Aprili, mwaka huu akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mkutano huo ambao Kaulimbiu yake ni “Kuelekea Mustakabali wa Pamoja” utafanyika chini ya Uenyekiti wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa Theresa May na utafunguliwa na Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.
Majadiliano ya Mkutano wa CHOGM 2018 yatajikita kwenye maeneo manne makuu ya kipaumbele ambayo yatajadili namna Jumuiya ya Madola inaweza kufikia mustakabali wenye ustawi zaidi; mustakabali endelevu zaidi; mustakabali wenye haki zaidi; na mustakabali wenye usawa zaidi.
Mijadala katika maeneo hayo ya kipaumbele itahusisha masuala mbalimbali ikiwemo, kukuza zaidi biashara na uwekezaji baina ya nchi za Jumuiya ya Madola kwa manufaa ya nchi wanachama na Jumuiya nzima; kukuza na kuendeleza misingi ya demokrasia; ajenda ya mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo endelevu pamoja na masuala ya uhalifu wa kimataifa kama vile ugaidi, uhalifu wa kimtandao na usafirishaji wa binadamu.
Jumuiya ya Madola ilianzishwa mwaka 1949 kupitia Tamko la London ambalo lilikuwa ni matokeo ya Mkutano wa Mawaziri Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Madola.  Jumuiya ya Madola ina wanachama 53 ambapo kati ya hizo, nchi 19 ni za Afrika, 7 ni kutoka Asia, 13 ni kutoka nchi za Carribean na Mabara ya Amerika, 11 ni kutoka eneo la Pacific na nchi 3 ni kutoka Ulaya.
Ujumbe wa Makamu wa Rais unajumuisha Mheshimiwa Dkt. Balozi Augustine Mahiga (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki.
Makamu wa Rais na ujumbe wake wanatarajia kurejea nchini Aprili 22, mwaka huu.
Imetolewa na:
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
15/4/2018

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...