Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, DKT. AKINUMWI ADESINA, ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu hapa nchini kwa mwaliko wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kuahidi kuwa benki yake itawekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 1 nukta 5 kwenye sekta mbalimbali katika kipindi cha miaka miwili ijayo,

Dkt. Adesina ameyasema hayo alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, na kupokelewa na mwenyeji wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.

“Tunajivunia uhusiano wetu wa muda mrefu na Tanzania ambayo ni mnufaika anayeongoza miongoni mwa nchi za kiafrika kupata ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu kutoka benki yetu ambapo tangu mwaka 1971, Benki imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.6” alisema Dkt. Adesina

Alisema kuwa miradi inayoendelea hivi sasa nchini Tanzania kupitia ufadhili wa Benki yake imefikia thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2 ambapo uwekezaji mkubwa uko katika sekta za nishati ya umeme, usafiri, miundombinu ya barabara, kilimo, maji na usafi wa mazingira, kusaidia Bajeti Kuu ya Serikali pamoja na uendelezaji wa rasilimali watu.

“Katika miundombinu ya barabara peke yake, Benki yangu imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.1 na kwamba uwekezaji huo utasaidia kuboresha usafirishaji wa bidhaa na abiria hivyo kuchochea ukuaji na uendelezaji wa uchumi wa viwanda” alisema Dkt. Adesina.

Dkt. Adesina ameutaja mradi mwingine mkubwa wa kusafirisha umeme wenye msogo wa kilovolti 400 wenye njia yenye urefu wa kilometa 670 katika Ukanda wa Kusini na Kusini Magharibi mwa Tanzania, unaohusisha pia ujenzi wa vituo vya kupozea umeme katika mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga, wenye thamani ya dola milioni 220.

“Miradi hii pamoja na ile wa umeme wa kutumia joto ardhi pamoja na maji inayotarajiwa kupatiwa fedha na Benki hiyo, itasaidia sana mkakati wa Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, ambaye ammwagia sifa kwa utendaji kazi wake mahili, wa kujenga uchumi wa viwanda kwa kuwa na umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu” aliongeza Dkt. Adesina.
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, akizungumza jambo wakati Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika -AfDB, Dkt. Akinumwi Adesina (kushoto) akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pia anatarajiwa kuhudhuria Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mjini Dodoma. Katikati ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb).
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika -AfDB, Dkt. Akinumwi Adesina (kulia) akisisitiza jambo alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kupokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pia anatarajiwa kuhudhuria Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mjini Dodoma. kulia ni mwenyeji wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango. 
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika -AfDB, Dkt. Akinumwi Adesina (kulia) na mwenyeji wake Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) wakigonga “tano” wakati wa mazungumzo yao wakati rais huyo alipowasili nchini kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pia anatarajiwa kuhudhuria Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mjini Dodoma.


Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika -AfDB, Dkt. Akinumwi Adesina (kushoto) na mwenyeji wake Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) wakiondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, tayari kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambapo pia anatarajiwa kuhudhuria Maadhimisho ya Miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mjini Dodoma. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...