Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Ndugu Wallace Karia ametoa salamu za pongezi kwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na ile ya chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa kufuzu katika michezo yao iliyochezwa jana huko DR Congo na Burundi.

Ngorongoro Heroes wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za Africa za Vijana chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger mwezi Novemba baada ya ushindi wake wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Tanzania wakati Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka 17 inayoendelea huko Burundi.

Rais wa TFF Ndugu Karia amesema kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni faraja kubwa kwa Tanzania na inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea kuwekeza kwenye soka la vijana.Amesema Vijana hao wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada kubwa na wanastahili pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za mabenchi ya ufundi ya timu hizo.

“Tumepokea matokeo ya Vijana wetu wa Ngorongoro na Serengeti Boys kwa furaha kubwa kwasababu tumekuwa tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ambayo yanaonekana uwanjani kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea sifa kubwa Tanzania kwa ujumla” alisema Karia.

Aidha Rais wa TFF Ndugu Karia amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia maandalizi mazuri zaidi timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yanayowakabili.

Amesema TFF inajivunia vijana hao ambao wanaonesha mwanga mkubwa na amewaomba watu mbalimbali,Taasisi,makampuni kuunga mkono jitihada za TFF na kuiga mfano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojitokeza na kuisaidia Ngorongoro Heroes katika safari yake ya kwenda DR Congo kwenye mchezo wa marudiano.

Amemalizia kwa kuwashukuru wote wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira wa Tanzania huku akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao kwa TFF.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...