*Ofisa Mtendaji Moshingi aipongeza Serikali kwa uamuzi wa benki hiyo kuunganishwa na Twiga Bancorp

Na  Said Mwishehe, Blogu ya Jamii
BENKI ya TPB Pls imesema imeweka rekodi nzuri ya utendaji katika kipindi cha miaka 6 iliyopita ambapo hadi sasa mtaji wake umeongezeka kutoka Sh. bilioni 8 mwaka 2010 hadi kufikia zaidi ya Sh.bilioni 60. 

Imefafanua aidha  kwa mwaka 2017, benki ya TPB ilitoa gawio la zaidi ya Sh. bilioni moja kwa Serikali ambaye ndiye mwenye hisa nyingi. 

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo Sabasaba Moshingi wakati anatoa shukrani zake kwa Serikali kutokana na uamuzi wake wa kuamua kuiunganisha benki hiyo na pamoja na Benki ya Twiga Bancorp.

Akifafanua kuhusu benki hiyo amesema katika kuendelea kutekeleza majukumu yao benki ya TPB kwa mwaka 2017 ilipata faida kabla ya kodi ya Sh.bilioni 18.4 ikilinganishwa na faida ya Sh.bilioni 15.7 iliyopatikana mwaka 2016. 

Amesema matokeo hayo ya awali kwa robo ya kwanza ya mwaka 2018 inaonyesha mwaka huu faida inaweza kuongezeka zaidi ya kiwango cha mwaka jana.

"Tunatoa shukrani kwa Serikali ya awamu ya tano kwa kutuamini benki ya TPB kwa kazi tunayofanya kwa raia wa Tanzania, na tunahaidi tunaongea ufanisi zaidi, na kuwafikia walengwa wote katika jamii yetu,"amesema.

Kuhusu benki hiyo kuunganishwa na benki ya Twiga Moshingi amesema Mei 17 mwaka huu Benki Kuu ya Tanzania(BoT) kwa niaba ya Serikali, imeamua kuziunganisha benki hizo na kuunda benki madhubuti itakayojulikana kama benki ya TPB na kusisitiza kuunganishwa kwa benki hizi mbili kunatokana na kutetereka kwa mtaji wa benki ya Twiga. 

Moshingi amesema anaishukuru Serikali kwa kuiamini benki ya TPB pamoja na menejimenti yake, na kuamua kuziunganisha benki hizo ili kupata benki moja yenye nguvu na kuongeza ufanisi. 

Amesema kuunganishwa kwa benki hizo kunazaa benki moja imara ya TPB Bank Plc, ambapo wafanyakazi, wateja, amana pamoja na rasilimali zote zilizokuwa za Twiga Bancorp zitahamishwa kwenda TPB Bank Pc.

"Nachukua fursa hii kuwatoa hofu wateja wote waliokuwa na amana zao kwenye benki ya Twiga kuwa wasiwe na hofu kwani amana zao ziko salama kabisa, na wataendelea kupata huduma zote za kifedha kupitia kwenye matawi yao ya Twiga kwa muda, wakati taratibu zinafanyika ili kupata huduma hizo kwenye matawi yetu benki ya TPB mara baada ya taratibu ya kuunganishwa kwa mifumo ya benki hizi mbili utakapo kamilika,"amefafanua.

Moshingi ameongeza kuwa hata hivyo mashine za kutolea fedha za benki hizo mbili ziko kwenye mtandao mmoja na hivyo wateja wake wote wataendelea kupata huduma kama kawaida.

 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB Pls Sabasaba Moshingi (kushoto) akifafanua jambo jijini Dar es Salaam leo wakati akitoa shukrani  kwa Serikali kutokana na uamuzi wa kuinganisha benki hiyo na Benki ya Twiga Bancorp.Kulia ni Mkurugenzi wa Teknohama na Uendeshaji wa Benki ya TPB Jema Msuya.
Mkurugenzi wa Teknohama na Uendeshaji wa Benki ya TPB Pls Jema Msuya(kushoto) akibadilisha mawazo na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo leo jijini Dar es Salaam baada ya Ofisa Mtendaji Mkuu wao Sabasaba Moshingi kumaliza kikao kati yake na waandishi wa habari ambacho kilikuwa na lengo la kutoa shukrani zao kwa Serikali kwa uamuzi wa kuiunganisha benki hiyo na Twiga Bancorp.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...