Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

SHEIKH wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum amesema vijana wa Kiislamu ambao wamefunga ndoa wakati wa kuelekea mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wanatakiwa kupongezwa na kupewa moyo badala ya kuwabeza na kuwakejeli kwa uamuzi wao wa kufunga ndoa.

Sheikh Alhad ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumzia mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao umeanza leo kwa waumini wa dini hiyo kuanza kutekeleza moja ya nguzo za Kiislamu.

Hivyo wakati anazungumza mfungo huo, waandishi wa habari walitaka kupata maoni yake ni kwanini ndoa nyingi zinafungwa wakati wa kuelekea mwezi wa Ramadhan ambapo ametumia nafasi hiyo kufafanua ndoa ni kitu kitukufu na hakuna sababu ya kuwabeza wanaofunga ndoa.

"Kwanza kabisa naoMba muheshimu kitu kinaitwa ndoa kwani ni kitu cha heshima sana na binadamu anapotaka kuongeza nasaba yake lazima itapatikana kupitia ndoa.Ifahamike kuna ndoa na tendo la ndoa na yule ambaye anafanya tendo la ndoa bila ndoa hana tofauti na mnyama.

"Hivyo wanaofunga ndoa ni aina ya toba, mtu ambaye ameamua kufunga ndoa maana yake ameacha zinaa na hilo ni jambo jema.Mtu ambaye ameamua kuacha zinaa anatakiwa kupongezwa na hao wanaofunga ndoa kwenye mwezi wa Shaaban huenda imetokana tu na taratibu za mipango kukaa vibaya na inapofika karibu na Ramadhan anaona bora tu afunge ndoa na hiyo ni kwa kuheshimu tu mwezi wa Ramadhan,"amesema Sheikh Alhad.

Amesisitiza hakuna sababu ya kuwabeza wanaooa kwenye pindi cha kuelekea Ramadhan na wala hapaswi kukatishwa tamaa bali wanatakiwa kupewa moyo na hata ile kauli ya kusema ni ndoa za uji si vizuri.

Sheikh Alhad amesema vijana hao wanatakiwa kupewa moyo kwa kutafuta hifadhi ya ndoa na kueleza hata wanaosema ndoa nyingi ambazo zimefungwa kipindi cha kuelekea mwezi wa Ramadhan huwa zinavunjika baada ya mwezi kwisha hazina ukweli wowote.

Wakati huohuo amezungumzia umuhimu wa waumini wa dini ya Kiislamu katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan kuhakikisha wanajiepusha na mambo yasiyompendeza Mungu huku akisisitiza funga si kujiuzuia kula na kunywa tu bali ni kujizuia na mambo yote yasiyofaa.

"Funga macho yako kwa maana ya kuyazuia kutooa mambo yasiyo faa, funga mikono yako kwa maana ya kutopokea rushwa na kushika vitu vyenye kumchukiza Mola, funga miguu yako kwa maana ya kutokwenda kwenye mambo yasiyo na tija kiimani na hakikisha unafunga mdomo wako kwa kujiuzuia kutoa lugha chafu.Kipindi cha mwezi wa Ramadhan ni muhimu kufanya toba na yote yaliyomema,"amesema Sheikh Alhad.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...