*Sasa waomba kukutana naye ili wamueleze malalamiko yao

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

TUMESIKITISHWA kupuuzwa kwa maagizo ya Waziri Mkuu!Hiyo ndio kauli ya Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA) kwa madai licha ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra), kukutana na wadau wa usafiri kujadili malalamiko mbalimbali lakini hadi sasa wameshindwa kufanya hivyo.
Taboa wamedai Waziri Mkuu Majaliwa Mei 10 mwaka huu akiwa Bungeni alitoa maagizo kwa Sumatra kukutana na wadau wa usafirishaji  kwa lengo la kujadili na kupata ufumbuzi wa malalamiko yao yakiwamo ya faini kubwa  wanazotozwa wamiliki wa mabasi kwani imekuwa kero na kusababisha kuifanya shughuli hiyo kwa hasara.

Katibu Mkuu wa Taboa amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa kitendo cha Sumatra kuendelea kukaa kimya bila kuitisha kikao kimewavunja moyo na wanasikitika kuona maagizo yaliyotolewa yameshindwa kufanyiwa kazi huku wao wakitozwa faini kubwa ambazo wamezilalamikia muda mrefu.

"Tulitarajia baada ya maagizo tungeitwa wadau wa usafirishaji ili tujadiliane kwa pamoja na kupata muafaka badala ya kuendelea kukaa kimya. Sisi tumeendelea kuumia kwa kutozwa faini kubwa.Ombi letu ni moja tu hizi faini haramu ambazo zinatutesa ni vema zikaachwa kwanza hadi Sumatra watakapotuita.

 "Kwanza kanuni ambazo wanazitumia kututoza faini tunaziita haramu kwani wakati wa mchakato wake hatujashirikishwa na kibaya zaidi tukaona tu zinaanza kutumika.Kwa sasa matumaini yetu ni kwa Waziri Mkuu na hivyo ombi letu kwake tuaomba kumuona ili atusikilize, imani yetu tutapata muafaka na haya manyanyaso ya Sumatra yatakwisha,"amesema Mrutu.

Amesisitiza Mrutu kuwa kwa muda mrefu Taboa wamekuwa katika kusigana na Sumatra kuhusu sheria ya makosa mbalimbali iliyopitishwa Bungeni  waliyodai kutozingatia usawa na hivyo kuathiri utendaji wao katika sekta hiyo.

"Tunashumkuru Waziri Mkuu kwa kauli yake aliyoitoa bungeni kwani ameelezea hali halisi ilivyo kati yetu na Sumatra na akaomba wadau wote wa usafirishaji tuitwe ili kutafuta ufumbuzi wa yale ambayo tunayalalamikia,"amesema.

Katika mkutano huo wa Bunge unaoendelea, Waziri Majaliwa alisema mgogoro uliopo baina ya Sumatra na Taboa  unaohusu faini mbalimbali wanazotozwa wasafirishaji, ulishafika katika Ofisi yake, ambapo aliagiza Sumatra kukaa chini na Taboa na kupitia upya kanuni za uendeshaji ili kufikia muafuaka, jambo ambalo halijatekelezwa na Sumatra hadi sasa.

 Kwa kukumbusha tu Waziri Mkuu aliamua kutoa maagizo hayo kutokana na swali la Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Singida Martha Mrata, kumuuliza ni mgogoro uliopo kati ya Taboa na Sumatra  utamalizika ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara ya Taboa hadi kufikia hatua ya kuitisha migomo.

"Waziri Mkuu alijibu swali hilo la mbunge na kutoa maagizo wiki mbili mbili zilizopita lakini hakuna hatua ambazo zimechukuliwa.Kinachoendelea kwa sasa ni kulipishwa faini kubwa ambazo ndizo tunazilalamikia,"amesisitiza Mrutu.

Awali wasafirishaji hao waliilalamikia Sumatra kwa hatua yake ya kuandaa kanuni bila kuwashirikisha na baadae kuipeleka Bungeni na kuwa sheria, ambayo pamoja na  mambo mengine inawapa maumivu  ya kuwatoza faini kuanzia Sh 20,000 hadi Sh 500,000 kwa makosa ambayo kimsingi hayawahusu.

Mrutu amefafanua wanachotaka haki iwe inatendeka pindi yanapotokea makosa ya barabarani , lakini ni jambo la kushangaza hata kosa ambalo linafanywa na dereva lakini adhabu inakwenda kwa mmiliki na kusisitiza dawa ya kuondoa ajali ya barabarani si faini pekee yake,hivyo wakae wajadiliane.

Alipoulizwa iwapo ombi lao la kukutana na Waziri Mkuu limepokelewa Mrutu amesema ni mapema mno kulizungumzia suala hilo lakini ifahamike tu wameomba kumuona na wanaamini watakubaliwa kwani nia yao ni njema na ndio maana wamekuwa na subira.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...