Na Miza Kona, Maelezo-Zanzibar 

Kamati ya Kuangamiza Dawa za kulevya Zanzibar, imeangamiza kilo 38 za mihadarati aina heroini na vidonge vya valium ambazo zilikamatwa kuanzia mwaka 2010.

Zoezi la kuangamiza dawa hizo limefanyika leo katika jaa la Kibele, Wilayaya Kati.Kabla ya hatua ya kuzingamiza, dawa hizo zilikuwa zikitumika kama vielelezo vya ushahidi katika mahakama na vituo vya polisi kisiwani Unguja, ambapo sasa kesi zake zimemalizika na kutolewa hukumu.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kuangamiza dawa za kulevya ambae pia ni Mfamasia Mkuu wa Serikali Habibu Ali Sharif, amesema zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na hakuna athari yoyote iliyotokea wakati lilipotekelezwa.Aidha amesema, kamati yake inaendelea kuangalia uwezekano wa kuangamiza dawa kama hizo hapo baadae katika sehemu zilikopatikana badala ya kuzipeleka kwenye jaa la Kibele.

Alisema hatua hiyo inalenga kudhibiti uingizaji na utumiaji, pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji.Sharif aliitaka jamii kubadilika na vijana kuacha tabia ya kuiga mambo yasiyokuwa na tija, na badala yake wafuate maadili ya asili ya nchi yao ili waweze kuwa raia wema wa kulijenga taifa.Aidha amewahimiza wazee umuhimu wa kukaa na watoto wao na kuwapa mafunzo kuhusiana na mwenendo sahihi wa kuishi bila kujiingiza kwenye vitendo na biashara haramu za dawa za kulevya.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Abdalla Hassan Mitawi, amesema serikali imekuwa ikichukua hatua za kuwasaka, kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watu wanaoingiza, kusambaza na kuuza dawa hizo hatari ili kukinusuru kizazi cha sasa na baadae.

Aidha amefahamisha kuwa, baada ya zoezi hilo, serikali itatoa taarifa juu ya utekelezaji wake, ikilenga kubaini kama kuna watendaji wanaofanya udanganyifu katika utendaji ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Bi. Kheriyangu Mgeni Khamis, amesema zoezi hilo ni la pili kufanyika ambapo mwezi uliopita kamati iliangamiza dawa za kulevya aina ya bangi.

Zoezi la uangamizaji dawa za kulevya linakwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya kupambana na dawa za kulevya duniani inayofikia kilele Juni 26, 2018.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO-ZANZIBAR.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...