Na Mathias Canal-WK, Igunga-Tabora

Waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba ameshtushwa na wanawake pekee kuwa kwenye mashamba wakivuna pamba ilihali waume zao wakiwa kwenye Chang’aa (Pombe za kienyeji) ama kwenye vijiwe kupiga soga.

Dkt Tizeba ameshtushwa na wanawake wengi kuwa shambani wakivuna pamba ilihali waume zao wakiwa kwenye vijiwe vya pombe za kienyeji mara baada ya jana 18 Juni 2018 kutembelea katika Kijiji cha Bukama na Mwakipoleja vilivyopo katika kata ya Mbutu Wilayani Igunga Mkoa wa Tabora kujionea hali ya mavuno ya zao la pamba.

Waziri wa Kilimo Mhe Tizeba amesema kuwa kwa muda mrefu imekuwa kama utamaduni wa kawaida kwa wanaume katika maeneo mengi nchi kuwatelekeza wake zao wakati wa kuvuna pamba lakini wakati wa mauzo wanawake hao huachwa nyumbani pasina kujua kiasi kilichopatikana baada ya mauzo.

Hata hivyo wananchi wengi ambao ni wakulima wa pamba kijijini hapo wameishukuru Serikari kwa kuweka mfumo mzuri wa ununuzi wa zao hilo, ambalo kwa mwaka huu linauzwa kupitia katika minada inayosimamiwa na Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS).

Pia wakulima hao wameiomba Serikali kuziwezesha AMCOS kuwa na maghala makubwa na ya kisasa ya kuhifadhia pamba, lengo likiwa ni kuhakikisha pamba inahifadhiwa kwenye maeneo salama na kuifanya isipoteze ubora.

Mkulima wa pamba Ndg Elius Bushia kutoka kijiji cha Bukama alimueleza waziri wa kilimo kuwa awali kabla pamba kuanza kuuzwa kupitia AMCOS suala la ubora lilikuwa halizingatiwi na wakulima wengi kwani pamba yake ikikataliwa na kampuni moja alikuwa na uhuru wa kuipeleka kwenye kampuni nyingine hivyo jambo hilo lilichangia kupunguza ama kuisha thamani ya zao hilo.

Hata hivyo ameiomba Serikali kuwajengea uwezo viongozi wa Ushirika ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu na pia isaidie kutoa elimu kwa wanachama juu ya umuhimu na faida za AMCOS ili wakulima wengi waweze kujiunga.

Dkt Tizeba aliwaahidi wananchi hao kuwa changamoto zilizojitokeza kwenye kilimo mwaka huu serikali itazifanyia kazi ili kuzipunguza au kuzitokomeza kabisa huku akiwatangazia neema wakulima hao kuwa serikali itatoa mbegu na dawa za pamba bure ili wakulima wanufaike na matunda ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli.
Waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akishiriki uvunaji wa zao la Pamba, wakati alipotembelea Kijiji cha Mwakipoleja kilichopo kata ya Mbutu Wilayani Igunga Mkoani Tabora akiwa safarini kuelekea Mjini Dodoma, Jana 17 Juni 2018. Picha zote Na Mathias Canal-WK
Waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba akimkabidhi Felista Elius pamba aliyovuna, wakati alipotembelea Kijiji cha Bukama kilichopo kata ya Mbutu Wilayani Igunga Mkoani Tabora akiwa safarini kuelekea Mjini Dodoma, Jana 17 Juni 2018.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...