"Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na mume wake Mohamed Mpakanjia zinasema kwamba Mhe. Amina  Chifupa- Mpakanjia ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es Salaam amefariki dunia  majira ya saa tatu kasorobo - Juni 26, 2007...."

Hiyo ndiyo habari kuu iliyotawala vyombo vyote vya habari nchini na kuitikisa Tanzania na Watanzania ambao wengi walishindwa kuamini masikio na macho yao wakati TV, Magazeti, Redio na mitandao vilipokuwa vikitangaza  habari hiyo ya kusikitisha na kustua.

Amina Chifupa, ambaye alikuwa  mtangazaji maarufu sana wa kituo cha Clouds 88.5FM, hasa kwa vipindi vyake vya "Chei Chei Shangazi" na "Aftrika Bambaataa", aliingia bungeni baada ya kushinda nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kupitia tiketi ya Umoja wa Vijana wa CCM. 

Katika kipindi chake cha kifupi cha takriban miaka miwili  Bungeni, Marehemu alijizolea umaarufu mkubwa sana kwa  hoja zake nzito sio tu za  kutetea maslahi ya vijana na kukemea rushwa, bali pia kwa kuamua 'kumshika nyati mapembe'  kwa kupambana na janga la madawa ya kulevya kwa nguvu zake zote. Hadi sasa hajatokea  tena mbunge aliye shupavu kama yeye wa aliyekemea na kusema kwa sauti janga hilo la Taifa.

 Kwa bahati mbaya Amina Chifupa aliaga dunia  siku ya kilele cha Maadhimisho ya Kupambana na Madawa ya Kulevya Duniani, Juni 26. Hivyo ndio kusema kwamba, wakati Tanzania inaadhimisha siku hiyo Jumanne  huko mkoani Iringa, Wananchi pia watakuwa wanaadhimisha kumbukumbu ya miaka 12 ya kifo cha Amina Chifupa wa Mpakanjia. Unaweza ukaiita  AMINA CHIFUPA DAY.

Marehemu Amina alizaliwa Mei 20, 1981 jijini Dar es Salaam, alisoma Shule ya Msingi Ushindi, Mikocheni, Dar (1988-1994) kabla ya kujiunga na masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Wasichana ya Kisutu, Dar (1995-1998). Elimu ya Juu ya Sekondari alisoma katika shule ya Makongo (1999-2001) kabla ya kujiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Royal (2001-2003) ambako alifuzu Diploma ya Uandishi wa Habari.
Mwaka 1999 alianza kazi ya utangazaji wa kituo cha redio cha Clouds FM cha jijini Dar na aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mama Shughuli.  
Katika siasa alikuwa kada wa CCM, Kamanda wa CCM wa Umoja wa Vijana katika tawi la Mikocheni A jijini Dar, Katibu wa Kamati ya Uchumi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa wa Dar, Mama Mlezi wa UVCCM na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) matawi ya Bunju na Mbagala.
Mwaka 2005 aliteuliwa kuwa mbunge akiwakilisha kundi la vijana kupitia CCM ambako alidumu na cheo hicho kwa muda mfupi  hadi mauti yalipomkuta Juni 26, 2007.
Amina Chifupa alizikwa Juni 28, 2007 kijijini Lupembe Wilayani Njombe mkoa wa Iringa (sasa ni mkoa a Njombe) karibu kabisa na eneo alilokuwa akiishi bibi yake. Mazishi yake yalihudhuriwa na watu wengi maarufu wakiiongozwa na aliyekuwa Spika wa Bunge wa wakati huo Samwel Sita, ambaye pia ni marehemu.
Miaka mitatu baadaye, aliyekuwa mume wa  marehemu Amina Chifupa, Mohamed 'Medi' Mpakanjia, naye alifariki  dunia. Wawili hao walijaaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume anayeitwa Abdulrahman anayejulikana zaidi kama Rahman.
Baba mzazi wa marehemu Amina Chifupa, Mzee Hamisi Chifupa aalifariki  dunia usiku wa kuamkia Mei 27, 2017  nyumbani kwa mwanaye wa kike, Upanga, jijini Dar es Salaam.
Amina Chifupa daima atakumbukwa kwa kujitolea kupambana na matajiri wanaofadhili au kujihusisha na uingizaji wa dawa za kulevya nchini. Alikuwa mbunge mdogo zaidi katika historia ya chombo hicho cha  kutunga sheria na kupitisha bajeti ya nchi yetu.
Alisimama kidete na kutamka bayana angewaweka hadharani vigogo wote wanaojihusisha na madawa ya kulevya, pia alienda mbali zaidi kwa kutamka hata kama angekuwa mume wake anahusika naye angemtaja. Alikuwa jasiri kiasi hata  alifikia uamuzi wa kuwasilisha majina ya vigogo waliokuwa wakifanya biashara hiyo ya “unga” makao makuu ya Jeshi la Polisi Jijini Dar es Salaam.
Aliamua kujitoa mhanga kutetea kizazi cha vijana kinachoteketea kwa kutumia madawa ya kulevya ilihali waoingiza wanazidi kuwa matajiri tishio na baadhi yao wana nguvu ya ushawishi katika nyanja mbalimbali serikalini.
Alikuwa ni hazina kwa taifa na mfano kwa vijana wenye umri mdogo kama wake kwamba inawezekana kujitoa pasipo woga kulitetea taifa na kuwaweka wazi wote wanaotumia utajiri wao, vyeo vyao kufanya au kuwezesha uhalifu hususani katika suala zima la madawa ya kulevya. 
Lakini maskini ya Mungu ndoto yake hiyo na nyinginezo zilikatizwa ghafla na mauti saa tatu za usiku wa Juni 26, 2007 siku ya Jumanne katika hospitali kuu ya Jeshi ya Lugalo jijini Dar es salaam.
Mola aiweka mahali pema peponi roho ya marehemu Amina Chifupa wa Mpakanjia. WOTE NA TUSEME.... AMINA!

Kusoma yote tuliyoandika kumhusu Amina Chifupa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...