Na WAMJW - DSM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya kuingia kwa ugonjwa wa Chikungunya nchini baada ya watu wanne waliotokea  nchini Kenya kubainika kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa  huo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu mapema leo jijini katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam wakati akiongea na waandishi wa Habari.
“Mnamo tarehe 20, Mwezi Juni, 2018 wasafiri wanne wa familia moja waliotokea tena Mombasa nchini Kenya walishukiwa kuwa na ugonjwa huu baada ya kuwa na dalili zinazofanana na ugonjwa wa homa ya Chikungunya kwenye kutuo cha mpakani cha Holili kilichopo wilayani Rombo mkoani Kiliamanjaro”, alisema Mhe. Ummy
Waziri Ummy aliwatoa hofu wananchi kuwa Ugonjwa huu si mpya katika nchi yetu kwani hapa nchini  uligundulika katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania, sehemu za Makonde katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji mnamo mwaka 1952 huku  Jina la ugonjwa likiwa na asili ya Kimakonde lenye maana ya “kilichopinda” yaani  hali ya kupinda mwili inayotokana na maumivu makali ya viungo kunakosababishwa na ugonjwa huu.
Kwa upande mwingine Mhe. Ummy alithibitisha juu ya kuwepo kwa ugonjwa wa Dengue nchini hususani katika jiji la Dar es salaam huku idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226 ambao wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam.
‘Dengue ulithibitishwa kuwepo hapa nchini hususani jijini Dar es Salaam kuanzia mwishoni mwa mwezi wa Januari 2018. Hadi kufikia sasa idadi ya wagonjwa ambao wamethibishwa kuwa na ugonjwa huu kwa kipindi cha Januari hadi Mei ni 226 ambao wanatoka katika mkoa wa Dar es Salaam.  Vilevile ugonjwa huu si mpya hapa nchini kwani umewahi kuripotiwa katika miaka ya 2010, 2013 na 2014” alisema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy ameeleza dalili za ugonjwa wa Dengue zinashabihiana amabazo ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza kujitokeza siku ya 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya magonjwa haya. Wakati mwingine dalili za magonjwa haya yanaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa malaria. Vilele mara nyingine magonjwa haya yanaambatana na kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia kwenye njia ya haja kubwa au ndogo.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amethibitisha kuwa hadi sasa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola, huku kwa tathmini ilifanyika na Shirika la Afya Duniani (Regional Risk Assessment) imesema kuwa Tanzania ipo kwenye uwezekano wa kupata ugonjwa wa Ebola na imewekwa katika kundi la pili miongoni mwa nchi 6 zilizo katika hatari ya kupata maambukizi zaidi, kutokana na kupakana na nchi ya DRC pamoja na mwingiliano mkubwa wa watu wake.

Pia Mhe. Waziri amewatoa hofu Wananchi na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwani mpaka sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuugua ugonjwa huu hapa nchini, huku akiwaonya wanaosambaza taarifa za uzushi juu ya uwepo wa ugonjwa huu na kuwataka waache haraka.

Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Sekta mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kuendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti ili ugonjwa huu usiingie nchini na kuendelea kutoa taarifa pamoja na Elimu kwa Jamii kadri itakavyohitajika.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akieleza jambo mbele ya Waandishi wa Habari (Hawapo kwenye picha) wakati akitoa tamko kuhusu ugonjwa wa Chikungunya, Dengue na Ebola katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es salaam. Kushoto kwake ni Katibu mkuu wa Wizara ya Afya Idara Kuu ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya na Kulia ni Mkurugenzi Mkazi kutoka shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Adiele Onyeze.
 Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbali mbali wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu kuhusu ugonjwa wa Chikungunya, Dengue na Ebola katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...