Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wasikubali kuchonganishwa na kwamba Serikali haiongozwi kwa misingi ya kidini bali imeziachia taasisi za kidini zifanye kazi kwa kuzingatia Katiba , Sheria za nchi na malengo yaliyokusudiwa katika uanzishwaji wake. 
 Aliyasema hayo jana jioni (Jumamosi, Juni 9, 2018) alipozungumza na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza baada ya kushirikiana nao katika futari aliyowaandalia. Shughuli hiyo ilihudhuriwa na waumini wa dini mbalimbali. 
 Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, jambo litakalowawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu, hivyo wasikubali kuchonganishwa kwa misingi yoyote. 
 “Nawaasa viongozi wa dini msikubali kutumia makundi mengine nje ya taasisi zenu kwa ajili ya kuwazungumzia masuala yenu kwa sababu watawachonganisha na Serikali ambayo haipo kwa ajili ya kugombana na taasisi yoyote,” alisisitiza. 
 Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa la taasisi za kidini ni kuhakikisha wanawalinda waumini wao pamoja na kuwaongoza kwa kuwapa mafundisho mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu, ambayo yatawawezesha kuishi kwa amani . 
 Alisema misingi ya amani na utulivu ikiwa pamoja na mshikamano walionao wananchi umesababisha Tanzania kupata heshima kubwa dunia kote, hivyo ni vema kila mwananchi ahakikishe suala la kudumisha amani linapewa kipaumbele. 
 Pia Waziri Mkuu alisema amefurahi sana kujumuika na wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika futari hiyo, ambapo aliwapongeza kwa kukamilisha uundaji wa kamani za amani kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa.
 Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella amlishukuru Waziri Mkuu kwa ukarimu wake kwa kuwaalika wakazi wa Mwanza katika hafla hiyo, ambapo alisema Mwanza ni kitovu cha amani kwa kanda ya Ziwa na nchi za Maziwa Makuu. T
 “Mwanza tumejipanga na tunashirikiana na taasisi zote kwenye njanja zote , tupo pamoja na tunashirikiana katika kuimarisha amani na utulivu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kutuamini na tunamuahidi tutafuata falsafa zake katika utendaji wetu,”. 
 Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza na Askofu wa Kanisa la Charismatic Episcopal Church of Tanzania (CECT), Charles Sekelwa alisema wao wanaiunga mkono Serikali katika kudumisha amani na wataendelea kushirikiana nayo. 
 Alisema awali kulikuwa na changamoto ya matabaka ya kidini iliyobabisha na kutoelewana baina ya waislamu na wakiristo, ambapo kamati yao ilifanya kazi ya kuyasulisha na sasa hali ni shwari. “Matabaka ya kiimani yameisha na watu wa dini zote wanashirikiana vizuri,”
Askofu Sekelwa alisema wao kama viongozi wa pande hizo mbili hawawezi kukubali kuona kunakuwa na matabaka ya kiimani miongoni mwa waumini, hivyo watakikisha wanaendelea kuwafundisha waumini wao umuhimu wa amani. 
 Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Akson, Naibu Waziri waNchi, OR – TAMISEMI, Joseph Kakunda, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza
 Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha wakati alipowasili kwenye viwanja vya Benki Kuu jijini Mwanza kushiriki katika futari iliyoandaliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Juni 9, 2018. 
 Sehemu ya wakazi wa jiji la Mwanza wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza katika futari aliyoiandaa kwenye viwanja vya Benki Kuu jijini Mwanza Juni 9, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofuturisha kwenye viwanja vya Benki Kuu jijini Mwanza Juni 9, 2018. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika dua iliyoongozwa na Sheikh Khamis Almasi (wanne kushoto) baada ya kufuturisha kwenye viwanja vya Benki Kuu jijini Mwanza Juni 9, 2018.  Wengine kutoka kushoto ni Naibu Waziri TAMISEMI, Joseph Kakunda, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Jamal Abdul Babu na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani inayojumuisha  viongozi wa dini zote ya mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akigana na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani inayojumuisha viongozi wa dini zote ya mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekela baada ya kufuturisha kwenye viwanja vya Benki Kuu jijini Mwanza Juni 9, 2018.  Wengine kutoka kushoto ni Naibu Waziri TAMISEMI, Charles Kakunda na  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na Sheikh Khamisi Almasi. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu baada ya kufuturisha kwenye viwanja vya  Benki Kuu jijini Mwanza Juni 9, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...