THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

MASHAHIDI KATIKA KESI INAYOMKABILI TIDO MHANDO KUENDELEA KUSIKILIZWA JULAI 18

Na Karama Kenyunko, blogu ya Jamii

 MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mkurugenzi mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando utaendele kusikilizwa Julai 18 mwaka 2018.

Ushahidi dhidi ya kesi hiyo ulipaswa kuendelea kusikilizwa leo Julai 11 mwaka huu lakini Wakili wa Takukuru, Leonard Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu , Huruma Shaidi kuwa shahidi waliyemtarajia atoe ushahidi amepatwa na udhuru hivyo akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine.Kutokana na taarifa hiyo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 18 mwaka huu kwa mashahidi wa upande wa mashtaka kuendelea kutoa ushahidi.

Katika kesi hiyo tayari mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi ambao ni Ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh.milioni 887.1

 Anadaiwa kuwa Juni 16, 2008,   akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa mkurugenzi wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.

Pia anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake kwa kusaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl. Agosti 11,mwaka  2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, mshtakiwa alisaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Pia anadaiwa kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Inadaiwa kuwa, kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh. 887,122,219.19.