Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama amempa mwezi mmoja mkandarasi anayejenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa kilometa mbili inayounganisha Daraja la Nyerere na barabara ya Kibada-Feri iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam, kukamilisha kazi  hiyo hadi tarehe 31 Agosti, mwaka huu, ili kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wanaovuka daraja hilo.
Waziri Mhagama ameyasema hayo wakati akikagua  ujenzi wa barabara hiyo na kujionea uendeshaji wa shughuli  katika daraja la Nyerere, ambapo amefafanua kuwa kutokamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kunasababisha kero  kwa wananchi wanaovuka kwa miguu na wanaotumia vyombo vya usafiri kushindwa kupita kwa urahisi, hali inayochangia kupungua kwa mapato yanayokusanywa darajani hapo.
“Hii barabara ni ya msingi kwani kutokamilika kwake ndo maana hata magari madogo hayapendi kutumia hii njia, Mkandarasi huyu ameomba mara mbili kuongezewa muda kukamilisha kazi hii na sasa tunampa muda tena, nataka kazi hii ikamilike kwani baada ya  kukamilisha ujenzi wa daraja hili tulitegemea kuwa mapato tutakayo kusanya hapa yatatuwezesha kulipa gharama tulizotumia kuwekeza na kujenga daraja hili, lakini nimejaribu kuangalia makusanyo ya tangu mwaka 2016/2017 na mwaka 2017/2018 inakuwa kidogo sana ikilinganishwa na mapato ya mwaka 2016, hili lazima liangaliwe,   tunataka daraja hili liendelee kutoa huduma na liendelee kuleta faida kwenye mfuko na ukizingatia fedha hizi ni za wanachama zilizotumika” Amesema Mhagama.
Waziri Mhagama amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuhakikisha unawekwa mfumo bora wa utambuzi wa vyombo vya usafiri vinavyovuka darajani hapo ili kujua gharama halisi ya tozo kwa vyombo vya usafiri vinavyovuka darajani  hapo na kuepuka upotevu wa mapato kutokana na kutokuwa na mfumo wenye kutambua tozo halisi kwa vyombo hivyo.
“Nataka Mkurugenzi ushughulikie kwa haraka sana mfumo wa utambuzi wa vyombo vya usafiri vinavyovuka hapa. Tumejifunza mfumo wa malipo ni wa kielektroniki lakini utaratibu wa  utambuzi wa vyombo vya usafiri vinavyovuka hapa kwa kuangalia tu kwa macho na uhakika huo wa tozo kwa chombo cha usafiri inategeea sana na huyo mkadiriaji, lazima tuwe na utaratibu wa mfumo mzuri wa kielekroniki wa kufanya kazi hii ili tuweze kujipima vizuri katika ukusanyaji wa mapato tunayo kusanya hapa bila hivyo tutakuwa tunapoteza mapato mengi” Amesema Mhagama.
Kwa upande wao Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), William Erio na na Mkandarasi wa barabara hiyo, Mhandisi Jamal Mruma wote kwa pamoja
wamemuhakikishia Waziri Mhagama kutekeleza maagizo hayo kwa wakati ili kuondoa usumbufu uliopo kwa sasa kwa wananchi wanaotumia  daraja hilo  na kuweza kuongeza makusanyo ya mapato yanayotokana na tozo za vyombo vya usafiri vinavyovuka katika daraja hilo.
Barabara hiyo inajengwa na Kampuni ya China Railway Construction Agency Group, kwa gharama ya shilingi bilioni 21.1, ambapo tayari kampuni hiyo imeshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 10.5. Kukamilika kwa barabara hiyo kutaongeza mapato yanayotokana na tozo za vyombo vya usafiri vinavyovuka Darajani hapo ambapo tangu Daraja hilo lianze kufanya kazi mwezi Mei, 2016 hadi Juni 2018,  takribani shilingi bilioni 17.1 zimekusanywa na kwa wastani kila mwezi mapato ya shilingi milioni 600 hukusanywa.
 Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akimueleza jambo Mhandisi Jamal Mruma, anayejenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa  kilometa mbili inayo unganisha Daraja la Nyerere na barabara ya Kibada -Feri iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati akikagua ujenzi wa daraj hilo. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. William Erio
 Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Bw. William Erio wakimsikiliza  Mhandisi Jamal Mruma, anayejenga kwa kiwango cha lami barabara yenye urefu wa  kilometa mbili inayo unganisha Daraja la Nyerere na barabara ya Kibada -Feri iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati akikagua ujenzi wa daraj hilo.
Mmoja wa Wananchi akikamilisha taratibu za malipo katika Daraja la Nyerere lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam. Daraja la kigamboni tangu lianze kufanya kazi  mwezi Mei mwaka 2016 hadi Juni 2018, takribani shilingi bilioni 17.1 zimekusanywa na  kwa wastani kila mwezi mapato ya shilingi milioni 600 hukusanywa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...