WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amempokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon ambaye amewasili nchini leo saa 12:30 jioni (Jumamosi, Julai 21, 2018) kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

Kwenye uwanja wa ndege, Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Korea alipokelewa pia na Waziri wa Mambo ya Nje, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack Kamwele, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Lee Nak-yon anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.

Pia ameambatana na ujumbe wa maafisa wa Serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa ambao watashiriki Kongamano la Kibiashara baina ya Korea na Tanzania (Korea-Tanzania Business Forum) lililopangwa kufanyika kesho kutwa (Jumatatu, Julai 23, 2018) kwenye hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.

Kesho (Jumapili, Julai 22, 2018), Waziri Mkuu Lee Nak Yon atakuwa na mazungumzo rasmi ya kiserikali na mwenyeji wake pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali na pia kwa pamoja watashuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa watu wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi (diplomatic and service passports).

Pia ataenda Ikulu kumsalimia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, atatembelea Makumbusho ya Taifa, Hospitali ya Mnazi Mmoja na kituo cha utunzaji taarifa cha NIDA kilichopo Kibaha. 

Anatarajiwa kuondoka nchini Jumatatu jioni, Julai 23, 2018. 


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 21, 2018.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Lee Nak-Yon wakati mgeni huyo alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Julius Kamabarage Nyerere jijini Dar es salaam kwa ziara ya kikazi ya siku tatu chini Julai 21, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mheshimiwa Lee Nak- Yon baada ya mgeni huyo kuwasili kwenye  uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam kwa Ziara ya siku tatu nchini, Julai 21, 2018.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...