Na Zanzibar Leo 
 RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amemtambulisha winga wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars. Karia amemtambulisha Amunike mwenye umri wa miaka 47 katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam jana baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili. 
 Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, mtihani wake wa kwanza utakuwa ni mchezo dhidi ya Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
 Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga. Mayanga aliiongoza Taifa Stars kwa mara ya mwisho Machi 27, mwaka huu ikishinda 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
Taifa Stars inakuwa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017. 
 Zaidi ya hapo, Amunike amefundisha klabu za Al Hazm ya Saudi Arabia, kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 alipojiunga na Ocean Boys, zote za Nigeria. 
 Alipoachana na U-17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda wengi, Taifa Stars. 
 Kisoka, Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya. 
 Alianza na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I’Cons ya Korea Kusini alikocheza hadi 2004 kabla ya ku
hamia Al-Wehdat ya Jordan kumalizia soka yake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...