Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inaendelea kutoa huduma ya kupandikiza figo ambapo hadi hivi sasa tayari wagonjwa 19 wamenufaika na huduma hiyo tangu ilipoanzishwa kwa mara ya kwanza hapa nchini  Novemba mwaka 2017.
Utoaji wa huduma hiyo ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambayo ili elekeza kuweka mipango thabiti ya kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ambayo yalikuwa hayatolewi hapa nchini ama kutokana na wataalam wa kutoa huduma hizo au vifaa vya uchunguzi.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Hedwiga Swai alipokua akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Prof. Lawrence Museru kuhusu  upandikizaji figo.
“Tunapenda kuwafahamisha kuwa wagonjwa wote tuliowapandikiza figo pamoja na ndugu zao waliojitolea figo wanaendelea vizuri na shughuli zao kama kawaida. Hii inaonesha ni kwa kiwango gani huduma hii imefanikiwa tangu ilipoanzishwa Novemba mwaka jana ”. amesema Dkt Swai.
Akifafanua amesem zoezi hilo la upandikizaji  figo limeshirikisha wataalamu wazalendo toka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya BLK, Taasisi ya Saifee iliyopo Mumbai India pamoja na Hospitali ya kimataifa ya Sakra ya nchini India.
“Tunapenda kuwataarifu kuwa katika kutoa huduma hii, tayari wataalamu wetu wa ndani hususani Madaktari bingwa wa upasuaji wamepata ujuzi wa kufanya upandikizaji wenyewe kwa kiwango cha asilimia 75 huku asilimia 25 wakielekezwa na wataalamu kutoka nje. Hii ni hatua kubwa sana katika kuongeza ujuzi wa kutoa huduma hiyo. Maeneo mengine tayari wamefikia asilimia 100 hususani wauguzi wa vyumba vya upasuaji, Madaktari bingwa wa tiba ya magonjwa ya figo (Nephrologists), wataalam wa vipimo vya maabara na Radiolojia.
Kwa mujibu wa Dkt. Swai MNH  itaendelea kufanya upasuaji kwa wagonjwa watano kila mwezi ikiwa ni mpango  wa muda mfupi katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kuanzia sasa ambapo mpango wa muda mrefu  ni kufanya upasuaji kwa mgonjwa mmoja kila siku sawa na wagonjwa 20 kwa mwezi ambapo watakuwa wagonjwa 200 hadi 240 kwa mwaka.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya figo Hospitali ya Taifa Muhimbili Onesmo Kisanga amesema utafiti uliofanyika Kaskazini mwa Tanzania unaonesha kwamba asilimia 6.8 wana matatizo ya ugonjwa wa figo. Hivyo amewashauri Watanzania kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka na kuepuka matumizi mabaya ya dawa bila ushauri wa Daktari ili kuepuka magonjwa hayo.
  Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt . Isaack Mlatie akitoa figo kwa ajili ya kupandikiza kwa mgonjwa mwenye tatizo la figo. Katikati ni daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mfumo wa Mkojo, Muhimbili, Dkt. Gabriel Mtaturu akishiriki katika upasuaji huo. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Upasuaji  wa Mfumo wa Mkojo kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Sakra nchini India, Dkt. Girish Nelivigi akishirikiana na madaktari wa Muhimbili kufanya upasuaji huo.

 Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Njiku Kim akiandaa figo kabla ya kupandikizwa kwa mgonjwa. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo wa Muhimbili, Victor Sensa akishirikiana na Dkt. Kim kuaandaa figo kwa ajili ya kupandikizwa kwa mgonjwa mwingine.
 Wataalamu wakiendelea na upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
 Wataalamu wa upasuaji wa mfumo wa mkojo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa upasuaji wa mfumo wa mkojo kutoka nchini India.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Muhimbili Dkt. Hedwiga Swai( katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo, kuhusu maendeleo ya upandikizaji figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kushoto ni Daktari bingwa upasuaji wa mfumo wa mkojo Njiku Kim , kulia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya figo Onesmo Kisanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...