NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO

Meli kubwa ya mizigo iitwayo MV RAHIMA (LAND CRAFT RAHIMA) imeungua moto kwa asilimia 20,katika bandari ya Bagamoyo,mkoani Pwani.

Meli hiyo inayomilikiwa na Hamis Rashid mkazi wa Unguja ilikuwa ikiongozwa na kapteni Abdulrahman Abdulaziz ambae ni mkazi wa Unguja na ina uwezo wa kubeba mzigo wenye ukubwa wa tani 500 kwa mara moja.MV RAHIMA imekaa kwa muda wa wiki moja katika bandari ya Bagamoyo ikisubiri kupakia mzigo wa mifuko ya saruji wa tani 300 na ndani ya meli kulikua na watu 16 ambao ni mabaharia na wafanyakazi wengine wa meli.

Akielezea chanzo cha moto huo ,kapteni wa meli hiyo Abdulrahman Abdulaziz alisema ni hitilafu ya umeme .“Mlango wa mbele wa meli ulikua umeharibika, hivyo alfajiri ya tarehe 14 agosti, tuliamkia kuutengeneza kwa kuuchomelea maana ulikua na hitilafu, tayari kwa kujiandaa kupokea mzigo na kuanza safari ya kurudi Unguja”alisema Abdulrahman.

Alielezea, wakiwa katika kutengeneza mlango huo, ghafla waliona moshi mkubwa eneo analokaa kapteni wa meli kuongoza meli, na hivyo kusitisha zoezi la kuchomelea mlango na kwenda kuangalia sababu ya moshi huo.Kwa mujibu wake, moto ulianzia katika chumba cha kepteni wa meli saa 11:45 asubuhi na taarifa ziliwafikia kituoni katika jeshi la zimamoto saa 12:25.

Alisema ,eneo ambalo moto umetokea lina vyumba sita vya abiria ambavyo vyote vimeungua, na wakati moto unaanza kulikua na mabaharia wawili vyumbani wamelala ambao wote wametoka salama.Alisema meli ya MV RAHIMA imesajiliwa Zanzibar na ina vibali vyote vya usajili, lakini vyote vimeungua moto katika ajali hiyo ya moto .

Hata hivyo, mhusika huyo hajui meli hiyo ilisajiliwa mwaka gani ila imefanyiwa ukaguzi mwaka huu Pemba lakini anakiri hajui ni lini hasa imefanyiwa ukaguzi huo kwa maana ya tarehe na mwezi na mamlaka iliyokagua meli hiyo haifahamu.
Kamanda wa zimamoto wilaya ya Bagamoyo, Hiward Mwanza alisema ,meli haina mlango wa dharura wa kutokea nje inapotokea ajali ama hatari.

Alisema, haina alama za zinazoonesha dharura mfano emergency exit na mfumo wa utoaji maji kwenye meli umeoza .” Mabaharia hawana mafunzo ya kujikinga na moto na meli hii haina vifaa vya zimamoto”alifafanua Mwanza.Kamanda wa polisi mkoani Pwani ,Jonathan Shanna alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Meli kubwa ya mizigo iitwayo MV RAHIMA (LAND CRAFT RAHIMA) ambayo imeungua moto katika bandari ya Bagamoyo,mkoani Pwani.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...