JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Ndugu January
Makamba (Mb), leo anaanza ziara ya mikoa 19 nchini, ambayo itafanyika
kwa awamu tatu. Ziara hiyo inamadhumuni yafuatayo:-
1. Kukagua,
kutathmini na kuzungumza na viongozi, wataalam, watendaji na wananchi
wa mikoa husika kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa
Sheria ya Mazingira.
Kama inavyofahamika, Sheria ya Mazingira,
hasa vifungu vya 47, 51, 54, 56, na 58 (3), inatoa mamlaka kwa Waziri
mwenye dhamana ya mazingira kutangaza, kutamka au kuamuru, kupita kwenye
Gazeti la Serikali, baadhi ya maeneo nchini kuwa ni Maeneo Lindwa
Kimazingira (Environmental Protected Area) au Maeneo Nyeti Kimazingira
(Environmental Sensitive Area).
Nyenzo
hizi zimewekwa ili kuyalinda maeneo muhimu kwa mifumo ya kiikolojia
(ikiwemo vyanzo vya maji, mito, maziwa, mabwawa, milima na vilima,
chemichemi, ardhi oevu, mazalia ya samaki, misitu, nk.) ambayo hayana
ulinzi wa Sheria nyingine. Sheria imeweka vigezo kwa maeneo hayo.
Ofisi
ya Makamu wa Rais, kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC), iliomba na kupokea kutoka katika Halmashauri
mbalimbali nchini mapendekezo ya maeneo hayo. Jumla ya maeneo 77
yalipendekezwa, ikiwemo vyanzo muhimu vya maji, mazalia ya samaki na
wanyama adimu, maeneo ya ardhi oevu, mabwawa, mito na chemichemi nyeti.
Mikoa iliorodhesha maeneo hayo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na
Sheria. Katika awamu ya kwanza, maeneo takriban 20 yanatarajiwa
kuhifadhiwa kwa kutumia Sheria ya Mazingira.
Katika ziara yake,
Ndugu Makamba anatarajia kuyaona maeneo hayo, kutathmini hoja na haja ya
kuyahifadhi na kuzungumza na viongozi wa mikoa, halmashauri na wananchi
katika maeneo hayo ilikubaini utayari na uwezo wao katika kusimamia
uhifadhi mara maeneo hayo yatakapotangazwa. Vilevile, katika ziara hiyo,
Ndugu Makamba atapokea mapendekezo ya maeneo mapya hasa pale ambapo
mapendekezo yaliyotolewa awali hayakutokana na ushirikishwaji mpana.
Orodha ya maeneo yanayopendekezwa itatolewa kadri ziara inavyoendelea
katika kila mkoa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...