Na Deodatus Kazinja

Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza nchini wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kujinufaisha na mali za Jeshi hilo kinyume na utaratibu.

Hayo yalisemwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo Phaustine Kasike wakati akizungumza na maafisa na askari wa gereza Mpwapwa na Kongwa kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kikazi katika vituo hivyo Agosti 14 mwaka huu.

Kamishna Kasike alisema si jambo la kificho kukuta shamba, mifugo na mali nyinginezo za gereza zinamilikiwa na kuendeshwa na mkuu wa gereza kama mali yake binafsi.

Mkuu huyo wa magereza nchini akionesha kukasirika alisema siyo siri kukuta shamba la mkuu wa gereza au mkuu wa magereza wa mkoa likiwa limestawi huku shamba la serikali limesinyaa kabisa kwa visingizio vya hali ya hewa wakati vyote viko sehemu moja na vinatumia nguvu kazi ya wafungwa na raslimali nyinginezo hizo hizo za serikali.

“Nawataka maafisa na askari ndani ya Jeshi la Magereza kutambua kuwa tabia za namna hii ndizo zimesababisha Jeshi letu kutosonga mbele. Tunatazamwa kama watu tulioshindwa kutimiza wajibu wetu kwa tabia zetu za udokozi, wizi na ubinafsi na tunaoweza kurekebisha hali hii ni sisi wenyewe” alisema Kamishna Kasike.

Akitolea mfano wa mifugo kama ng’ombe na mbuzi Jenerali Kasike alisema ni jambo la kawaida kukuta kituo kiko na idadi hiyo hiyo ya mifugo kwa miaka kadhaa bila kuongezeka mfugo hata mmoja na ikiwa kuna mabadiliko ni ya kupungua tena kwasababu ambazo hazina mashiko.

Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike (katikati) akikagua moja ya nyumba zinazojengwa kwa mtindo wa kujitolea gerezani Mpwapwa. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Salum Omari na wa kwanza kushoto ni mkuu wa Gereza Mpwapwa Mrakibu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Nobert Ntacho. 
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike (mwenye miwani) akikagua mradi wa ufyatuaji tofali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kuishi maafisa na askari kwa njia ya kujitolea. 
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike (wa kwanza kulia) akikagua shamba la mikorosho la gereza Mpwapwa alipofanya ziara ya kikazi gerezani hapo Agosti 13 mwaka huu. Shamba hilo lina ukubwa wa ekari 58 na kati ya hizo ekari 15 tayari zimeanza kutoa matunda. Kwa msimu wa mwaka 2017/18 zaidi ya kilo 2400 zilipatikana. 
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike akisalimiana na maafisa wa gereza Mpwapwa mkoani Dodoma alipowasili kituoni hapo kwa ziara ya kikazi Agosti 14,2018. 
Baadhi ya maafisa wa gereza Kongwa mkoani Dodoma wakifuatilia kwa makini hotuba ya Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike (hayupo  pichani) alipofanya ziara ya kikazi kituoni hapo Agosti 14, 2018. 
Kamishna Jenerali wa Magereza Phaustine Kasike (katikati) akiongea na baadhi ya maafisa gereza Kongwa (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi kituoni hapo Agosti 14, 2018.Wa pili kushoto ni Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza (SACP) Salum Omari. Wa kwanza kushoto ni Afisa Mnadhimu katika ofisi ya Mkuu wa Magereza mkoani Dodoma Kamishna Msaidizi wa Magereza Mwaruka Dugange, wa pili kulia ni Mkuu wa gereza Kongwa Mrakibu wa Magereza John Nyonyi na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Kambi Mkoka Mrakibu wa Magereza Felix Samson. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...