Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba amehidi kutoa mifuko hamsini ya saruji na bati hamsini kama mchango wake katika ujenzi wa Shule ya awali ya Kizimkazi iliyopo takiriban kilomita 61 kutoka Mjini Unguja. 

Ahadi hiyo ameitoa hii leo Shehia ya Kizimkazi- Mkunguni katika Wilaya ya Kusini, Jimbo la Makunduchi katika maadhimisho ya Siku ya Kizimkazi. “Nawapongeza sana kwa hatua hii mliyofikia na utayari wenu wa kuwekeza katika miradi mikubwa hususan elimu ambayo ndio nguzo kuu” Makamba alisisitiza. 

Waziri Makamba amewataka wana Kizimkazi kuandaa utaratibu wa kutembeleana na kubadilishana uzoefu baina yao na vijiji vya Tanzania Bara ili kudumisha Muungano na kujenga ushirikiano zaidi. “Mwakani tuweke nguvu zaidi, tuwe na vikundi vya ngoma na sanaa mbalimbali kutoka upande wa pili wa Muungano pia tutaanda ziara ya mafunzo ili kwa pamoja muweze kubadilisha uzoefu” alibainisha Makamba. 

Aidha, Waziri Makamba amewakumbusha wana Kizimkazi kuuenzi na kuulinda Muungano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa Muungano haukuanzisha undugu bali Muungano umerasimisha undugu baina yetu, na wakubainisha kuwa changamoto za Muungano zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi. 

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Shule hiyo Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Kizimkazi Bi. Rehema Ramadhani amesema kuwa Shule hiyo imeanza kujengwa kwa nguvu za wananchi na baadae kuungwa mkono na wadau mbalimbali. Bi Ramadhani amebainisha kuwa kumalizika kwa ujenzi huo itakuwa ni faraja kubwa kwa wazazi na wanafunzi kutokana na sehemu finyu na hatarishi katika jengo la awali kwa kuzingatia kuwa Shule hiyo ipo mkabala na barabara kuu. 

Aidha, imebainika kuwa tangu kuanzishwa kwa sherehe hizo za ‘Siku ya Kizimkazi’ wakazi hao wamefanikwa kujenga ukumbi wa shule kwa ajili ya kufanyia mitihani, ukarabati wa nyumba ya daktari, ujenzi wa nyumba ya mwalimu pamoja na ujenzi wa shule ya awali ambayo leo hii jiwe la msingi limewekwa. 

Sherehe hizi za Siku ya Kizimkazi huadhimishwa kila mwaka mara moja kwa lengo la kuthamini maendeleo pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo na kutafuta mbinu mbadala za utatuzi. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umoja wetu, Ushirikiano wetu na Mshikamano wetu ndio ngao yetu” 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba mara baada ya kuweka jiwe la Msingi wa ujenzi wa Shule ya awali ya Kizimkazi iliyopo Shehia ya Kizimkazi- Mkunguni katika Wilaya ya Kusini, Jimbo la Makunduchi –Unguja ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za siku ya Kizimzikazi. Katika kuchangia ujenzi huo Waziri Makamba atatoa mifuko 50 ya saruji na bati 50.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akisalimiana na watoto katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa Shule yao ya awali Kizimkazi. Kulia ni Mkurugenzi wa Uratibu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais – Zanzibar Bw. Khalid Hamran
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akihutubia wakazi wa Kizimkazi hii leo katika Shehia ya Kizimkazi- Mkunguni katika Wilaya ya Kusini, Jimbo la Makunduchi –Unguja ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za siku ya Kizimzikazi, sherehe zilizoenda sambamba na uwekekaji wa jiwe la msingi katika shule ya awali. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria na Utawala Bora Mhe. Haroun Ali Suleiman (katikati) akimkaribisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mhe. January Makamba kulia sherehe za Siku ya Kizimkazi, jimboni Makunduchi. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...