Frank Mvungi- MAELEZO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  amezindua Bodi  mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kuiagiza Bodi hiyo kutekeleza miradi ya kimkakati ili lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo litimie.
Akizungumza leo Jijini Dodoma katika hafla ya uzinduzi huo amesema kuwa wanachama wana matarajio makubwa na utendaji wa Bodi hiyo, hivyo jukumu lake ni kuhakikisha kuwa inafanya tathmini ya miradi yote iliyokuwa inatekelezwa na mifuko iliyounganishwa ili kuona namna bora ya kuiendeleza.
"Jukumu lenu kama Bodi ni kuhakikisha kuwa miradi kama ule wa Kiwanda cha kuzalisha viatu Karanga inaendelezwa kwa maslahi ya nchi yetu, sambamba na miradi yote ya kimkakati iliyopo ni vyema mkaharakisha mchakato wa kuifanya ianze mara moja kwa kuwa matarajio ya Serikali ni kuona mfuko huo unakuwa imara, endelevu na unatoa huduma bora ya Hifadhi ya Jamii"; Alisisitiza Mhe. Mhagama.
Akifafanua amesema kuwa sekta ya hifadhi ya Jamii imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii kwa kuwekeza shilingi Trilioni 11.79 katika vitega uchumi ikiwemo miundombinu, daraja la Kigamboni, Ujenzi wa Hospitali, Vifaa tiba na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
"Tekelezeni majukumu yenu kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, ushirikiano, nidhamu, uadilifu na weledi wa hali ya juu, uongozi wenu ndiyo utakaowezesha PSSSF kukidhi matarajio ya wanachama"; Alisisitiza Mhagama.
Akizungumzia uwajibikaji kwa menejimenti na wajumbe wa Bodi, Waziri Mhagama amewaasa kuzingatia sheria kanuni na taratibu za matumizi ya fedha na rasilimali za mfuko huo ili kuleta tija kama ilivyo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  akizungumza kuhusu umuhimu wa Bodi  mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kusimamia rasilimali fedha kwa kutekeleza miradi ya kimkakati katika mfuko huo wakati akizindua Bodi hiyo leo Jijini Dodoma.
  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Mhandisi Mussa Iyombe akisisitiza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuzindua Bodi  mpya ya Mfuko huo leo Jijini Dodoma.
 Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Eliud Sanga akitoa taarifa fupi ya utendaji kazi wa mfuko huo wakati wa hafla ya kuzindua Bodi mpya ya mfuko huo ambapo  tayari umeshafungua Ofisi katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Ofisi moja Tanzania Visiwani ikiwa ni moja ya hatua za kuwahudumia wanachama wake katika mikoa yote hapa nchini.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi  mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe leo Jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama  akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi mpya ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) mara baada ya kuzindua Bodi hiyo leo Jijini Dodoma. kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo Mhandisi Mussa Iyombe na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Eliud Sanga.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...