Mwakilishi wa Mufti Sheik Hassan Chizenga akimkabidhi tuzo ya kuthamini utendaji kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Agnes Kuhenga wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia walioko nchini kwa ajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa ambao valvu zao hazifanyi kazi vizuri. Kushoto ni Naibu Balozi wa Saudi Arabia Mhe. Ahmed Al Ghamidi.

Na Salome Majaliwa - JKCI 

 Huduma bora za matibabu pamoja na upasuaji wa moyo zimeifanya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutambulika kimataifa na hivyo wataalamu wengi kutoka nje ya nchi kuvutiwa kwenda kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo kwa kushirikiana na madaktari wa Taasisi hiyo. Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Mufti,Sheik Hassan Said Chizenga wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia ambao wako JKCI katika kambi maalum ya upasuaji wa moyo.

Sheik Chizenga alisema Taasisi ya Moyo imekua kimbilio kwa wagonjwa wa Afrika na Dunia nzima kwa ujumla kutokana na huduma bora za matibabu ya moyo zinazolewa kiufanisi.

“Taasisi hii imekua kioo si kwa Afrika tu bali Dunia nzima kwa kutoa huduma ya matibabu ya Afya ya moyo na upasuaji kwa wagonjwa ambao ni watanzania na wengine kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati” ,alisema Sheik Chizenga. Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Agnes Kuhenga aliishukuru nchi ya Saudi Arabia kwa ushirikiano inaouonyesha kwa Serikali ya Tanzania katika kuimarisha utaalam na kuboresha utoaji wa huduma za afya hapa nchini.

“Ushirikiano wa Tanzania na Saudi Arabia umelenga kuhakikisha watanzania wanakuwa na afya bora na kuweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kulifanya taifa letu kufikia lengo la kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025”, alisema Kuhenga.

Naye Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Ahmed Al Ghamidi alisema katika kambi hiyo wataalamu kutoka nchi zote mbili wameweza kuunganisha nguvu na ujuzi waliokuwa nao na kufanya matibabu kwa wagonjwa.

Mhe.Balozi Ghamidi alisema, “Katika kambi hii ya siku saba maisha ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji yameweza kuokolewa na pindi watakapopona watarudi nyumbani na kuendelea na majukumu yao ya kazi za kila siku”,.

Katika kambi hiyo jumla ya wagonjwa 20 wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na kubadilishwa valvu zaidi ya mbili ambapo hadi leo wagonjwa 14 walishafanyiwa upasuaji na hali zao zinaendelea vizuri.
Naibu Balozi wa Saudi Arabia Mhe. Ahmed Al Ghamidi akimkabidhi zawadi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga wakati wa hafla fupi ya kuwashukuru wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini humo walioko nchini kwa ajili ya kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa ambao valvu zao hazifanyi kazi vizuri. Kushoto Mwakilishi wa Mufti Sheik Hassan Chizenga.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kuhenga akimkabidhi tuzo ya kutambua kazi ya upasuaji wa moyo wanayoifanya kwa wagonjwa Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo pamoja na mishipa ya damu Khalid Kamal Alhroub kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia ambao wako JKCI kwa ajili ya kambi maalum ya matibabu ya moyo. Hadi sasa jumla ya wagonjwa 14 wameshafanyiwa upasuaji wa moyo na kubadilishwa valvu zaidi ya mbili.
Mwakilishi wa Mufti Sheik Hassan Chizenga akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Balozi wa Saudi Arabia Mhe. Ahmed Al Ghamidi, viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na wafanyakazi wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia mara baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kuwashukuru wataalam kutoka nchi hiyo ambao wako JKCI kwa ajili ya kutoa huduma ya matibabu ya moyo. Picha na JKCI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...