Na Mwandishi Wetu
MLEZI wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’, Dk. Reginald Mengi, amesema kuwa kikosi hicho kina kila sababu ya kufanya kweli katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kufanyika hapa nchini Aprili mwakani.
Mengi aliyasema hayo jana baada ya kutambulishwa rasmi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa mlezi wa timu hiyo, hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa TFF, Walace Karia, makamu wake, Athuman Nyamlani na Katibu wa shirikisho hilo, Wilfred Kidau.
Mwenyekiti huyo wa Makampuni ya IPP, alisema kuwa amefurahi mno kupewa nafasi hiyo ya kuwa mlezi wa Serengeti Boys, ukizingatia ni miongoni mwa wadau wa soka la vijana, akiwa ameifuatilia mno timu hiyo kwa muda mrefu.
“Hakuna sababu ya Serengeti Boys kutokuwa washindi, tunaamini tunaweza na timu hii itailetea Tanzania heshima kubwa. Shakira (mwanamuziki wa Colombia) aliimba ‘This time is for Africa’ wakati wa Kombe la Dunia 2010, na sisi tunasema ‘This time is for Tanzania (safari hii ni zamu ya Tanzania).
“Tuna kila kitu cha kutufanya tuwe washindi, wanachotakiwa vijana kufanya ni kujiamini. Tutafanya kila tunaloweza kuhakikisha timu inapata maandalizi ya kutosha ili iweze kufanya vizuri,” alisema.
Alimtaka kila Mtanzania kujivunia timu hiyo ya Serengeti Boys huku akiahidi kutowaangusha watanzania kutokana nafasi hiyo.
“Nawahakikishia Serengeti Boys itashinda mechi zote na kutwaa ubingwa,” alisisitiza Dk. Mengi.
Kwa upande wake, Karia alisema: “TFF tunafarijika kwa ndugu Mengi kukubali kuwa mlezi wa timu hii ya Serengeti Boys na tunaamini kwa pamoja tutaifanya timu hii kuwa msingi mzuri katika maendeleo ya ustawi wa soka la vijana.”
Alisema kuwa mkakati wao ni kuhakikisha timu hiyo inafanya vema katika michuano hiyo ikiwa kama mwenyeji, lakini pia kukinukisha kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Peru Oktoba mwakani na hata zile za mwaka 2026 nchini Mexico na Peru.
“Tunawaomba wadau wa soka nchini na viongozi mbalimbali kumuunga mkono Dk. Mengi katika majukumu yake hayo kwani itakuwa ni fedheha kwa Taifa kama wenyeji wa michuano iwapo ubingwa utatoka nje ya Tanzania,” alisema.
 Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd. Dk. Reginald Mengi (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika hafla fupi iliyofanyika ofisi za IPP ya kutambulishwa rasmi na TFF kuwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ jijini Dar es Salaam.  Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Wallace Karia. 
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Wallace Karia akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kumtambulisha rasmi Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd. Dk. Reginald Mengi (kulia) kuwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za IPP jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa Habari za Michezo Clouds TV, Jacob Mbuya (wa pili kushoto) akiuliza swali kwa mlezi wa timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, ‘Serengeti Boys’ Dk. Reginald Mengi (hayupo pichani) kuhusiana na malezi ya vijana hao ndani ya kambi na nje ya kambi wakati wa hafla fupi ya TFF kumtangaza rasmi kwa vyombo vya habari kuwa mlezi wa timu hiyo iliyofanyika katika ofisi za IPP jijini Dar es Salaam.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...