Zaidi ya asilimia 50
ya wakazi 8,000 wa Kata ya Ayamohe Wilayani Mbulu Mkoani Manyara,
waliokuwa hawapati maji safi na salama kutokana na kutokuwa na
miundombinu ya usambazaji wa maji ya uhakika wamefanikiwa kuondokana na
adha hiyo baada ya mradi wa maji kuzinduliwa. Akisoma taarifa ya
mradi huo wa maji jana kwenye mbio za mwenge wa uhuru, ofisa mtendaji wa
kata ya Ayamohe John Tluway alisema mradi huo umegharimu sh388
milioni.
Tluway alisema
serikali kuu imechangia sh322 milioni, halmashauri ya mji sh19 milioni
na serikali ya mtaa imechangia sh46 milioni kwa kutoa ardhi na kushiriki
kwenye uchimbaji mtaro na ulazaji mabomba ya kilomita 15.
Alisema baada ya
kukamilika kwa mradi huo wananchi wa eneo hilo hivi sasa watapata huduma
ya maji tofauti na awali walikuwa wanatembea umbali wa kilomita mbili
kufuata huduma hiyo.
“Lengo la mradi ni
kusogeza huduma ya maji karibu na na wananchi wa kata ya Ayamohe na
mitaa ya jirani inayowazunguka ili kuondoa upungufu mkubwa wa maji
unaosababishwa na ongezeko la wakazi,” alisema Tluway.
Awali, mkuu wa wilaya
ya Mbulu Chelestino Mofuga akisoma taarifa ya halmashauri ya mji wa
Mbulu alisema mwenge wa uhuru utatembea miradi sita ya thamani ya sh1.1
bilioni.
Mofuga alisema mwenge
utafungua mradi wa maji Ayamohe, uzinduzi wa kikundi cha wanawake cha
unenepeshaji ng’ombe na uzinduzi wa kiwanda cha usindikaji wa mikate na
biskuti. Alisema pia utakagua
shughuli za klabu ya wapinga rushwa shule ya sekondari Daudi, kuweka
jiwe la msingi kituo cha afya Daudi ufunguzi wa vyumba vinne vya
madarasa na choo cha wanafunzi na uzinduzi wa daraja la Endamaksi.
Mmoja kati ya wakazi
wa Ayamohe Jane Bayo alisema mradi huo wa maji utawanufaisha wananchi wa
eneo hilo waliokuwa wanatembea umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma
hiyo. Kiongozi wa mbio za
mwenge wa uhuru kitaifa kwa mwaka 2018 Charles Kabeho aliipongeza
halmashauri ya mji huo kwa kutekeleza mradi huo kwani wamefanikiwa
kumtwika mama ndo ya maji.
Askari upelelezi wa kituo cha polisi Mbulu, Gloria Nasson akielezea madhara ya matumizi ya dawa za kulevya huku akiwa ameshikilia bangi wakati mwenge wa uhuru ulipotembelea banda la polisi, kushoto ni Mkuu wa kituo cha polisi Mbulu, Amiry Mlemba.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Charles Kabeho akitambulishwa kwa Mkurugenzi wa Mji wa Mbulu, Anna Mbogo na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa, Charles Kabeho akizungumza baada ya kuzindua kiwanda cha usindikaji wa mikate na biskuti kwenye mtaa wa Gwandumehi Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Charles Kabeho akizindua kituo cha afya Daudi Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...