NaLilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
SERIKALI imetoa kibali cha kuajiri watumishi wapya 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wa Umma waliobainika kughushi vyeti.

Hayo yameelezwa leo Bunge, Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Capt. (Msataafu) George Mkuchika alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Aida Khenani kuhusu mkakati wa Serikali wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti feki.

"Vibali vya kuajiri watumishi hao vimetolewa katika ngazi ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waajiri wote wameendelea kujaza nafasi hizo, " alisema Mhe. Mkuchika.

Vilevile, amesema Serikali imetoa vibali vya ajira kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Kumb. Na. CFC.26/205/01/PF/91 cha tarehe 22 Agosti, 2017 na kibali Kumb. Na CFC.26/205/01/GG/95 cha tarehe 12 Machi, 2018 kuziba nafasi zote za Watendaji wa Vijiji na Mtaa zilizoachwa wazi kutokana na zoezi la kuhakikiwa vyeti kwa kuajiriwa watumishi wapya.

Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kutambua umuhimu kwa kuajiri watumishi wa kada mbalimbali Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 22, 150 wakiwemo watumishi wa kada za Ualimu 6,840, Fundi Sanifu wa Maabara za shule 160, kada za Afya 8,000, Wahadhiri wa Vyuo Vikuu 624 na watumishi 6,526 wa kada nyingine.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...