image001

UTANGULIZI 
 Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo uvunjaji sheria kwa baadhi ya kampuni au watu binafsi wasio na leseni za EWURA wanaonunua bidhaa za petroli (mafuta ya petroli, dizeli na taa) kutoka kwa kampuni za mafuta zinazoingiza na kuuza mafuta hayo kwa jumla (OMCs) na kuyauza mafuta hayo kwa wafanyabiashara wa rejareja wasio na leseni za EWURA. 
 EWURA inatoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaokiuka masharti ya biashara ya mafuta na kuwataka wafanyabiashara wote wa mafuta ya petroli nchini kuzingatia Sheria, Kanuni na masharti yaliyomo kwenye leseni zinazotolewa na EWURA. 

 UZINGATIAJI WA SHERIA WA 
BIASHARA YA BIDHAA ZA PETROLI 
 Kulingana na kifungu 131 cha Sheria ya Petroli Sura ya 392, hairuhusiwi mtu yeyote kufanya biashara ya mafuta ya petroli bila kuwa na leseni kutoka EWURA. Kanuni za biashara ya mafuta pamoja na masharti ya leseni za biashara ya mafuta kwa jumla zinazuia kuuza mafuta kwa kampuni nyingine au mtu yoyote isipokuwa kwa wafanyabiashara wenye leseni za kuendesha vituo vya mafuta na wale wenye leseni za kuhifadhi mafuta kwaajili ya matumizi binafsi. 

Kanuni za biashara ya mafuta pamoja na masharti ya leseni za kuendesha vituo vya mafuta zinazuia wafanyabiashara wa rejareja kununua mafuta kwa mtu yeyote yule isipokuwa kutoka kwa kampuni zenye leseni za kuagiza na kuuza mafuta kwa jumla (OMCs). EWURA pia imepewa jukumu la kusimamia/kuchochea ushindani katika sekta ya biashara ya mafuta hapa nchini. Wajibu huo umeainishwa katika Kifungu cha 30 (2) (k) (ix) cha Sheria ya Mafuta. 

ADHABU JUU YA UKIUKWAJI WA SHERIA 
 EWURA inafuatilia swala hili kwa karibu na inatoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaokiuka Sheria. 
EWURA itawatachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Sheria wale wote watakaobainika kuvunja Sheria. Kwa wale watakaotaka kupata ufafanuzi wowote juu ya Taarifa hii, wanaombwa kuwasiliana na ofisi za Makao Makuu ya EWURA, Dodoma au ofisi za EWURA za Kanda. 

 Imetolewa Na: MKURUGENZI MKUU 
 MAMLAKA YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA NISHATI NA MAJI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...