Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii

ALIYEKUWA  Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando amedai mchakato wa kuitoa TBC kwenye analogy kuingia kwenye digital ulifanywa na Bodi ya shirika hilo na kupata baraka za Bodi ya zabuni. 

Amedai mchakato huo ulitokana na maelekezo ya Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete ya kumtaka alibadilishe shirika  hilo lifikie katika hadhi inayostahili.

Tido amedai hayo leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alipokuwa akijitetea dhidi ya kesi inayomkabili ya matumizi mabaya ya madaraka.

Tido anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh.Milioni 887.1.

Amedai kuwa Serikali imewalipa Sh. Milioni hiyo 887.1 watu wasiojulikana badala ya mawakili kama inavyodaiwa  na upande wa Jamhuri

Akiongozwa na Wakili wake wa utetezi, Dk.Ramadhani Maleta, Tido amedai mwaka 2006 Rais Kikwete alimuita kuja kuiongoza TBC ambapo majukumu yake yalikuwa ni kulibadilisha shirika hilo liwe lenye uwezo na kuheshimika duniani. Amedai, tuhuma anazotuhumiwa nazo zimemuumiza sana kwa sababu alikuwa na ndoto ya kuifikisha TBC mbali ,ifikie kutoa gawio kwa Serikali na siyo serikali kutoa fedha kwa TBC.

Kuhusu kuisababishia Serikali hasara ya Sh.Milioni  887.1, Tido amedai kuwa, hakushirikishwa kwa namna yoyote katika malipo hayo na kwamba  angeshirikishwa angeweza kunusuru fedha hiyo isilipwe.

Alidai mwaka 2012 aliitwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU)  kutoa maelezo  na kwamba maalipo yanaonesha kufanyika mwaka 2015 wakati yeye akiwa tayari ni mtuhumiwa na hakuwahi kuitwa mahali popote kuulizwa kuhusu mchakato mzima wa mradi, kabla maalipo hayo hayajafanyika angeweza kushauri.

Tido amedai kwa taaluma yake ya uandishi wa habari kwa miaka 50 sasa, waliufahamu muda mrefu na kwamba wahusika wakubwa walikuwa ni TCRA na TBC kama shirika la Umma walikuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wake.
Amedai,  walishirikishwa katika vikao mbali mbali vya awali na kwamba wakati huo walipewa ishara ya maandalizi ya kuhakikisha wakati rasmi ukifika utekelezaji wa kuingia kwenye mfumo wa analogia unaanza ipasavyo.

Akiendelea kujitetea Tido alidai kuwa kwa kuangalia maeneo mengine shida kubwaza nchi za Afrika  nilikuwa ni kuwapatia watu kwenye uwezo wa kutekeleza mradi huo.

Amedai kutokana na ukubwa wa huo mradi, TBC ndiyo ilitegemewa kuwa inaongoza mradi huo hivyo iliruhusiwa kutafuta mmbia mwenye uwezo wa kifedha ili kusushirikiana naye  kuendesha mradi huo.

Tido alidai kuwa walitakiwa mwaka 2015 wahamie katika mfumo huo mpya wa digitali na kuwa  TBC  ili kufanikisha hilo walianza kuzungumza na watu  mbali mbali ambapo makampuni ya kimataifa yaliyokuwa na hadhi ambayo walikuwa wakiitaka yalikuwa machache na walikuwa na malengo ya kupata faida.

Tulifanikiwa kupata kampuni tatu kampuni ya Uswiss, kampuni ya Channel 2 group ya Dubai na kampuni ya Startimes nao walikuwa na matakwa yao mbalimbali.

Amedai, kampuni ya Uswiss walionesha mapema tayari wamepata nafasi nzuri Afrika Magharibi katika nchi za Nigeria na Ghana wakajiondoa na kwamba hata walipopelekewa mwaliko hawakujibu.

"Kampuni ya Channel 2 group wao walitaka kuhakikishiwa  kama watashirikishwa katika mchakato na kwamba wafanye makubaliano ya awali hivyo waliandikishana na kuwaambia utakapofika wakati wa mchakato wasiwe na wasiwasi.


Tido amedai, waliandikishiana na  katika maandishi hayo yeye alisaini na kwa upande wa Channel 2 group alisaini mmiliki wake Sethi Dubai na kwamba alifanya hivyo kwa kuzingatia  hayo ni makubaliano ya mwanzo.

Aliendelea kudai  wakati wa kushiriki katika mchakato ulipofika kampuni hizo mbili zilishirikishwa na kuwasilisha michanganuo yao na hatimaye kupatikana mshindi Star times. Amedai wakati wa mchakato wote huo ukiendelea a bodi ya TBC haikuwahi kulalamika  wala kutoa lawama zozote badala yake waliunga mkono jitihada hizo.

" Huu ulikuwa mradi wa mkubwa wa  kimataifa kwa hiyo bodi ya TBC waliamua kuuchukua mchakato mzima na kuuendesha na kuuondoa katika bodi ya zabuni ambayo inashirikisha wafanyakazi wa TBC na pia ilipata ushauri wa PPRA,"ameeleza Tido mahakamani hapo.

Amesema pia ilishirikisha taasisi nyingine kama TCRA, TIC, Wizara ya Mawasiliano, UDSM, Wizara ya Habari na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia, yalialikwa kwa kuleta wajumbe.

Alidai wataalam hao na kamati ya ufundi walikaa kwa siku mbili Bagamoyo kuchambua michanganuo iliyowasilishwa na kampuni za Channel 2 group na Star time kwa kina ili waweze kufanya maamuzi sahihi. Na baada ya kupitia kwa kina  makampuni hayo waliridhika wamejieleza inavyopaswa, na kwamba baadaye walipeleka majibu yao kwa bodi ambayo iliamua mbia wa TBC awe Startimes .

Tido amedai waliendesha vikao vingi ikiwamo kuandaa rasimu ya mkataba  ambayo walimpatia mwakilishi wa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali (AG) akaipitie neno kwa neno kama inakubalika na baadaye aliwaarifu inakubalika.

Alieleza kuwa Tanzania ilikamilisha mradi huo mwaka 2015 na kuwa nchi ya pili katika bara la Afrika na wataalam toka nchi mbalimbali wamekuwa wakijua kuona imewezekanaje na hadi hivi sasa bado kuna nchi za Afrika bado zinasuasua.

"Tangu nimekaa TBC sijawahi kupokea malalamiko yoyote toka kwa mmiliki wa Channel 2 Group Sethi, "ameongezaTido.

Akiendelea kutoa ushahidi wake, amedai, mkataba wake na TBC ulimalizika mwaka 2010, mchakato wa mabadiliko ya kutoka mfumo wa analoji kwenda digitali ulianza 2009 na kwamba hadi anaondoka alihakikisha umesimama kikamilifu.

Akiongozwa na Wakili  Matunda, Tido alioneshwa kielelezo kilichowasilishwa na upande wa mashtaka kwenye kesi hiyo ambacho kilioonyesha kuwa TBC, Serikali, AG na Wizara ya Habari waliipa kazi  kampuni ya uwakili ya Uingereza katika kesi ambayo ilikuwa ifunguliwe nchini humo.
Hata hivyo Wakili Matunda alimuonesha Tido vielelezo hivyo vya upande wa mashtaka  na risiti za malipo zilionesha mawakili hao wa Uingereza walitaka kulipwa Euro 280,603.57 huku TBC wakionesha mawakili hao walipwe Euro 434,226.21.

Tido amedai fedha hizo zinazodaiwa kulipwa kwa mawakili hao wa Uingereza na kusababisha hasara zililipwa kusikojulikana .

Hakimu Shaidi  aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9 mwaka huu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...