Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania na Shirika la Ndege Tanzania umeandaa Maonesho Maalum ya Utalii na kutambulisha rasmi kuanza kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania zitakazofanyika Mjini Mumbai nchini humo kuanzia mwezi Novemba, 2018. 
 Maonesho hayo ambayo yatafanyika kwenye miji mikubwa mitatau ya India yaani New Delhi, Ahmedabad na Mumbai yanalenga kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nnchini. 
 Akizungumza wakati wa maonesho hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya Roseate, Aerocity jijini New Delhi, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alisema kuwa anaona fahari kubwa kushiriki maonesho hayo muhimu kwa Tanzania na India.
Alitumia fursa hiyo kutangaza rasmi kuanza wa safari za kwanza za ndege ya shirika la ndege la Tanzania mjini Mumbai. Balozi Luvanda alisema kuwa safari za ndege hiyo nchini India ni fahari kubwa kwa Tanzania kutokana na ukweli kwamba nchi hizi mbili zina mahusiano ya kihistoria kwani mbali na kuunganishwa na Bahari ya Hindi, Tanzania na India ni marafiki na zimekuwa zikishirikiana katika Nyanja mbalimbali zikiwemo biashara, utamaduni na mawasiliano ya mtu mmoja mmoja. 
 Mhe. Balozi Luvanda alisisitiza kuwa, safari za ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania nchini India hususan katika mji wa Mumbai zitaimarisha sekta ya utalii nchini kwa kuongeza idadai ya watalii kutoka nchini humo ambao kwa sasa takribani watalii 40,000 kutoka nchini humo wanatembelea Tanzania kwa mwaka. 
 Pia zitarahisisha safari za wanafunzi wa kitanzania wanaosoma kwenye vyuo vikuu mbalimbali vya India ambao idadi yao imeongezeka na kufikia 2500 kwa mwaka. 
 “Ninayo furaha kubwa kuwajulisha kuwa shirika letu la ndege yaani Air Tanzania limefufuka. Na kuthibitisha hilo Shirika litaanza safari zake mjini Mumbai mwezi Novemba, 2018. Nawaomba msisite kutumia ndege yetu kwa safari zenu za utalii, biashara hata kwenda kusalimia ndugu zenu waliopo Tanzania na wale waliopo Tanzania kuja kusalimia ndugu huku India” alisisitiza Balozi Luvanda. 
 Mhe. Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wageni walioshiriki maonesho hayo ushirikiano, amani na usalama pale watakapokuwa Tanzania na kwamba Tanzania ni chaguo sahihi kwa utalii na wasisite kuja kwa shughuli mbalimbali za manufaa kwa nchi hizi mbili.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akizungumza wakati wa maonesho maalum ya utalii yaliyofanyika  katika Hoteli ya Roseate, Aerocity jijini New Delhi, India tarehe 17 Septemba, 2018. Mhe. Balozi Luvanda pamoja na mambo mengine alitumia fursa hiyo kutangaza kuanza rasmi kwa safari za Shirika la Ndege la Tanzania mjini Mumbai mwezi Novemba 2018. maonesho hayo yatafanyika kwenye miji mingine miwili ya India ambayo ni Ahmedabad na Mumbai.
Mhe. Balozi Luvanda akitangaza rasmi kuanza kwa safari za Shirika la Ndege la Tanzania nchini India huku  picha ya Ndege ya Shirika hilo aina ya Dreamliner ikionekana. Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Bi. Devotha  Mdachi ambaye yupo nchini India kushiriki maonesho hayo aliyoshiriki kuandaa anaonekana akichukua kumbukumbu ya tukio hilo
Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi Devotha Mdachi naye akizungumza wakati wa maonesho yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na Bodi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...