Serikali imetoa wito kwa wamiliki wa viwanda kuzingatia utekelezaji wa Sheria ya Mazingira na Mikakati mbalimbali iliyopo kwa ajili ya kuwezesha usimamizi endelevu wa hifadhi ya mazingira kwa faida yetu na ya vizazi vijavyo. 

Hayo yamesemwa leo bungeni Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima wakati wa kipindi cha maswali na majibu na kusisitiza kuwa Tanzania inachangia kiasi kidogo sana katika tatizo la uzalishaji wa gesijoto ambazo ndio chanzo cha mabadiliko ya   tabia nchi. Hata hivyo, pamoja na kuchangia kidogo kiasi hicho, Tanzania imeendelea kuathirika kutokana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi kama vile kupungua kwa barafu ya mlima Kilimanjaro, kuongezeka kwa usawa wa bahari; ukame, mafuriko ya mara kwa mara na mlipuko wa magonjwa.

Imebaini kuwa tatizo la mabadiliko ya tabia nchi kwa kiwango kikubwa linasababishwa na uzalishaji wa gesijoto unaotokana na matumizi ya nishati (47%), uzalishaji viwandani (30%) na usafirishaji (11%) kwa shughuli za maendeleo katika nchi zilizoendelea kiviwanda hususan za Ulaya, Amerika, Asia na Australia. Bara la Afrika kwa ujumla limechangia gesijoto kiasi kisichozidi asilimia    tatu (3). Tanzania huzalisha    kiasi cha tani 0.09 za hewa ukaa (Per Capital emission) kwa mwaka.

Mheshimiwa Sima amesema kuwa, tatizo kubwa linatokana na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na baadhi ya viwanda nchini ni kutiririsha maji taka yenye sumu  na kemikali ambazo huathiri sana viumbe hai pamoja na mazingira kwa ujumla.

 “Tanzania inayo Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004, Sheria hii imeweka misingi ya Usimamizi, Tathmini na Kuchukua tahadhari kuhusu madhara kwa mazingira yakiwemo ya viwandani. Kwa kuzingatia Sheria hii, Serikali imekuwa ikielimisha na kuwatoza faini wamiliki wa Viwanda wanaokiuka Sheria hii na wanaoendelea kukaidi maelekezo na masharti waliyopewa hufungiwa kufanya shughuli na kupewa masharti kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao tena.” Alisisitiza Mhe. Sima. 

Wakati huo huo Mhe. Sima amewataka wamiliki wa viwanda kote nchini kuhakikisha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (Environmental Impact Assessment) na Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit) vinafanyika na kuzingatiwa. Aidha, wamiliki wa viwanda wanapaswa kutumia nishati rafiki kwa mazingira na kutumia teknolojia banifu katika uzalishaji wa bidhaa zao ili kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima akitoa majibu ya Serikali wakati wa kipindi cha maswali na majibu hii leo Bungeni mjini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...