Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso ameelekeza Watalaam wa maji walioshiriki katika kusimamia ujenzi wa miradi ya maji ya Tsamas na mradi wa maji Darakuta-Minjingu pamoja na Wakandarasi waliopewa kandarasi katika miradi hiyo kufika katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Babati bila kukosa asubuhi ya tarehe 23.10.2018.

Mhe. Aweso (Mb) ambaye yuko mkoani Manyara katika ziara ya kikazi ametoa maelekezo hayo baada ya kubaini kasoro katika utekelezaji wa miradi hiyo ambapo pamoja na Serikali kutoa fedha, bado wananchi hawajapata huduma ya majisafi na salama.

Mradi wa maji wa Darakuta-Minjingu ambao hadi sasa umetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.7 ulisanifiwa mwaka 2009 na ulitakiwa kuhudumia vijiji vya Minjingu, Mwada, Ngoley, Olasiti, Masaini, Maramboi na Eluwai. Aidha, mradi wa maji wa Tsamas mkandarasi amelipwa zaidi ya Shilingi milioni 100, hata hivyo mabomba yaliyotumika katika chanzo cha maji yanapasuka hivyo kusababisha ukosefu wa huduma ya majisafi ya uhakika kwa wananchi.

Naibu Waziri Aweso (Mb), pamoja na hayo,  amepongeza utekeleza wa mradi wa maji wa Haraa unaozalisha lita elfu 21 kwa saa kwa kukamilika vizuri, na kuagiza fedha za mradi ziwekwe benki ili kuwezesha kamati ya watumia maji  kuendesha mradi.

Hadi mwezi Septemba 2018 mkoani Manyara, huduma ya upatikanaji maji vijijini ilikua asilimia 52 na Babati mjini asilimia 75.
 Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiongea katika eneo la mradi wa maji wa Bonga, uliopo kata ya Bonga Babati  mkoani Manyara. Mradi huo utakapokamilika utatoa maji lita elfu 40 kwa saa na kufikisha kiwango cha upatikanaji majisafi na salama katika mji wa Babati kuwa asilimia 95. Aidha, vijiji vya jirani navyo vitapata huduma ya majisafi na salama kupitia mradi huo. Waziri Aweso (Mb) amesema wote watakaostahili fidia kupisha mradi Serikali itawalipa.
 Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb)-kushoto, akimsikiliza Mbunge wa Babati vijijini Mhe. Jitu Soni –kulia, akimweleza kuhusu hali ya mradi wa maji wa Tsamas. Katikati ni MKuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Elizabeth Kitundu. 
 Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb)  aliyenyoosha mkono, akitoa maelekezo kuitwa popote walipo kwa Watalaam wa maji waliosimamia miradi ya maji ya Tsamas na mradi wa maji Darakuta –Minjingu, pamoja na Wakandarasi wa miradi hiyo mara moja.  Miradi hiyo imebainika kuwa na kasoro nyingi za kitalaamu, na haitoi maji ingawa Serikali imewalipa Wakandarasi
 Baadhi ya wanakijiji wa Kijiji cha Tsamas mkoani Manyara wakijadili kuhusu maji  katika kikao kifupi katika shamba la migombawakati wa ziara ya kikazi ya  Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) haonekani pichani.
 Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiangalia maji yanayochotwa  katika mto Tsamas kwa matumizi mbalimbali na wananchi. 
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akikagua ubora wa bomba zilizotumika katika mradi wa maji Darakuta-Minjingu. Mradi huo ulisanifiwa mwaka 2009, na umeshatumia kiasi cha shilingi Bilioni 1.7, hatahivyo wananchi bado hawajapata huduma ya majisafi na salama, hivyo wahusika wote, wakiwamo watalaam wa maji na wakandarasi wa mradi wameelekezwa kufika  katika kikao kitakachofanyika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Babati. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...