Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dr. Abdallah Possi, aliwasilisha hati za utambulisho kwa Rais wa Hungary Bw. János Áder hivi karibuni. Pamoja na Ujerumani, Ubalozi wa Tanzania uliopo Berlin pia unahudumia maeneo mengine tisa tisa ya uwakilishi, ikiwemo nchi ya Hungary. 
 Baada ya kuwasilisha hati, Balozi alipata fursa ya mazungumzo mafupi na Rais wa Hungary, mazungumzo ambayo yalilenga zaidi katika masuala ya kilimo, elimu na maji. 
Balozi Dkt. Possi alimueleza Rais wa Hungary kwamba Tanzania inawakaribisha wawekezaji katika maeneo mbalimbali, yakijumuisha pia viwanda vinavyojihusisha na mazao ya kilimo. Dkt. Possi alifafanua kwamba, kilimo ni sekta ambayo bado inategemewa na watanzania walio wengi, na kwamba kuna fursa nyingi zaidi katika sekta ya kilimo siyo tu kutokana na uwepo wa ardhi nzuri yenye rutuba, bali pia uwepo wa idadi kubwa ya watu ndani ya Tanzania na nchhi zinazoizunguka, hali ambayo inahakikisha uwepo wa soko la uhakika katika bidhaa za kilimo. 
Dkt. Possi aliongeza kwamba, uwekezaji wa kilimo siyo tu utapunguza upotevu wa mazao unaojitokeza baada ya mavuno, bali pia utasaidia uongezaji thamani ya mazao ya kilimo, na hivyo kuchagiza zaidi biashara ya mazao ya kilimo, na kuongeza ajira kwa idadi kubwa ya watanzania ambao wanategemea kilimo.
 Balozi Dkt. Possi pia aliishukuru serikali ya Hungari kufuatia mpango unaowapa fursa watanzania kupata elimu ya juu nchini Hungary. 
Rais wa Hungary Bw. János Áder alimueleza Balozi Dkt. Possi kuhusu mkutano mkubwa kuhusiana na masuala ya maji unaotarajiwa kufanyika nchini Hungary mwaka 2019, mkutano ambao utawakutanisha wataalamu wa maji kutoka nchi mbalimbali duniani. 
Rais Áder alisema mkutano huo ni fursa nyingine ya kufahamu aina mbalimbali za teknolojia zinazoweza kutumika kutatua changamoto kubwa ya upotevu wa maji. 
 Balozi Dkt. Possi pia aliweka shada la maua katika mnara wa mashujaa wa Hungary. Mnara huu ulijengwa kwa heshima ya askari wote wa Hungary waliofariki katika vita, na ambao miili yao haikupatikana au kutambuliwa. 
Siku moja kabla ya kuwasilisha hati za utambulisho, Balozi Dkt. Possi alikutana na jumuia ya Watanzania wanaoishi nchini Hungary. Dkt. Possi aliwapongeza watanzania hao kwani, licha ya idadi yao ndogo, wameonyesha moyo wa mshikamano, jambo ambalo ni muhimu kwa mshikamano thabiti wa jumuia za watanzania wanaoishi nje ya nchi. 
Pia Dkt. Possi aliwaeleza watanzania hao kwamba bado wana nafasi ya kupeleka maendeleo nyumbani, na kwamba milango ya Ubalozi wa Tanzania uliopo Berlin iko wazi kwa kila mtanzania anayeishi katika eneo linalohudumiwa na Ubalozi huo. Watanzania hao pia walipata fursa ya kuuliza masuali ambayo yalipatiwa majibu.
Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dr. Abdallah Possi, akiwasili katika kasri la Budapest tayari wasilisha hati za utambulisho kwa Rais wa Hungary Bw. János Áder hivi karibuni.
Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Dr. Abdallah Possi, akitambulishwa  katika kasri la Budapest  kabla ya kuwasilisha hati za utambulisho kwa Rais wa Hungary Bw. János Áder hivi karibuni.
 Baada ya kuwasilisha hati, Balozi alipata fursa ya mazungumzo mafupi na Rais wa Hungary, mazungumzo ambayo yalilenga zaidi katika masuala ya kilimo, elimu na maji.
Balozi Dkt. Possi pia akiweka shada la maua katika mnara wa mashujaa wa Hungary. Mnara huu ulijengwa kwa heshima ya askari wote wa Hungary waliofariki katika vita, na ambao miili yao haikupatikana au kutambuliwa. 
Balozi Dkt. Possi na mkewe na afisa wa ubalozi wakipozi baaada ya yeye kuweka  shada la maua katika mnara wa mashujaa wa Hungary. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...