Na. WFM Mjini Bali Indonesia

Marekebisho ya Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2018, hayawazuii wadau wa takwimu kutoa takwimu kwa ajili ya matumizi yao bali marekebisho hayo yanaweka misingi ya kuzingatiwa wakati wa utoaji wa takwimu hizo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango, alipofanya mkutano na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha (IMF) anayewakilisha Tanzania na nchi nyingine (Africa Group 1 Constituency), Bw. Maxwell Mkwezalamba, katika Mikutano ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mjini Bali Indoneshia.

Dkt. Mpango amesema kuwa lengo la marekebisho ya sheria hiyo ni kurahisisha ufanyaji wa tafiti na utoaji wa matokeo ya tafiti na sio kuwabana wadau katika ukusanyaji wa taarifa za kitakwimu au kuzuia mijadala ya uchambuzi wa kisera wa matokeo ya takwimu rasmi.

“Tumekubaliana kutumia fursa ya kuboresha Kanuni za Takwimu kwa ajili ya kuweka mazingira ya utekelezaji mzuri wa vipengele vya sheria vilivyorekebishwa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kuelewa lengo la marekebisho hayo”, alieleza Dkt. Mpango. Marekebisho hayo ya kanuni za takwimu yatawezesha utekelezaji mzuri wa vifungu vya sheria vilivyorekebishwa ambapo ametoa wito kwa wadau kushiriki katika mchakato wa marekebisho hayo.

Aidha, Waziri alieleza kuwa mwezi Novemba mwaka huu Serikali itakutana na wadau wa maendeleo, ili kutoa fursa kwa wadau hao kuelewa kwa kina dhumuni la Serikali kufanya marekebisho yaliyofanyika na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwezi Septemba 2018.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akielezea maboresho ya sheria ya takwimu inayowafanya watafiti waweze kufanya tafiti zao kwa urahisi kwa maendeleo ya taifa, wakati wa Mkutano kati yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeziwakilisha nchi za Afrika Bw. Andrew Bvumbe (hayupo pichani), wakati wa mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na Benki ya Dunia (WB) mjini Bali Indonesia, kushoto ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA Bw. Charles Kichere. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeziwakilisha nchi za Afrika Bw. Andrew Bvumbe (wa pili kushoto) akifurahia jambo kwenye mkutano na wajumbe wa Tanzania walioshiriki mikutano Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na Benki ya Dunia (WB) mjini Bali Indonesia. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Fedha na Mipango- Bali Indonesia) .
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed (kulia), akieleza kuhusu mpango wa kuboresha Sekta ya uvuvi ili kureta tija wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) anayewakilisha nchi za Afrika Bw. Maxwell Mkwezalamba (hayupo pichani), wakati wa mikutano ya mwaka ya IMF na Benki ya Dunia (WB) mjini Bali Indonesia. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) anayewakilisha nchi za Afrika, Bw. Maxwell Mkwezalamba, akiipongeza Tanzania kwa hatua iliyochukua ya kukuza uchumi, wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) uliofanyika Mjini Bali Indonesia. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeziwakilisha nchi za Afrika, Bw. Andrew Bvumbe (kulia), akieleza jambo wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (wa pili kushoto), wakati wa mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa- IMF na Benki ya Dunia (WB) mjini Bali Indonesia, wa tatu kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed na kushoto ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania- TRA, Bw. Charles Kichere. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...