Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akizungumza na Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Prof. Zacharia Mganilwa wakati wa mazungumzo baina yao leo Ijumaa Jijini Dar es Salaam kuhusiana na mikakati mbalimbali ya Chuo hicho kwa ajili ya kuboresha tasnia ya mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amekipongeza Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kuandaa programu ya ufadhili wa masomo ya uhudumu wa ndege kwa washindi wawili wa mashindano ya urembo ya Miss Tanzania. Akizungumza jana Ijumaa (Oktoba 19, 2018) Jijini Dar es Salaam na Viongozi wa Chuo hicho, Dkt. Mwakyembe alisema Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano na kuunga mkono juhudi za NIT, na kuahidi kufanya mawasiliano taasisi mbalimbali za ikiwemo Shirika la Ndege Nchini (ATCL) ili kuchangamkia fursa hiyo.

Dkt. Mwakyembe alisema programu ya mafunzo hayo, yatasaidia kuongeza tija na thamani ya mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania kwani kwa sasa yatapitia katika mchujo wa kuwapata washindi waliojengeka katika mmaarifa na weledi wa kitaaluma.

“Sasa hatutakuwa na sababu ya kuhangaika kutafuta wahudumu wa ndege, NIT mmekuja na programu inayounga mkono mageuzi makubwa katika Shirika letu la ndege la ATCL na hivyo sehemu pekee ya kupata wahudumu wa ndege zetu ni kupitia mchakato wa mashindano ya Miss Tanzania” alisema Dkt. Mwakyembe.

Aidha Dkt. Mwakyembe alisema Serikali itaendelea kuhamasisha  taasisi mbalimbali za Serikali ili kuhakikisha kuwa mkakati huo wa programu ya mafunzo ya NIT  yanaungwa mkono tija katika kuchagiza mageuzi ya kimkakati katika sekta ya Uchukuzi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Akifafanua zaidi, Dkt. Mwakyembe alisema malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kuanzia mwakani mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania yanaanza kuzalisha mabalozi wa lugha ya Kiswahili, ikiwa ni kielelezo cha utambulisho wa Mtanzania katika eneo lolote duniani.

“Kati ya lugha 6000 duniani, Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa na watu wengi zaidi na kwa mujibu wa Utafiti ya Umoja wa Afrika, ifikapo mwaka 2063 lugha ya Kiswahili itakuwa lugha ya utambulisho wa mtu mweusi, hivyo hatuna budi kujivunia lugha yetu adhimu ya kiswahili” alisema Dkt. Mwakyembe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha NIT, Prof. Zacharia Mganilwa alisema Taasisi yake imeamua kufanya mageuzi ya kimkakati katika mitaala ya Chuo hicho ili kwenda sambamba na Mageuzi ya Sekta ya Uchukuzi yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.

Aliongeza kuwa katika mwaka wa masomo 2018/19, Chuo hicho kimeanza kutoa mafunzo ya programu ya uhudumu wa ndege yenye jumla ya wanafunzi wa 24, ambapo inafundishwa kwa kipindi cha miezi mitatu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...