Imeelezwa kuwa maboresho ya miundombinu ya skimu ya kilimo cha umwagiliaji ya Igomelo iliyopo wilayani Mbarali Mkoani Mbeya, imewanufaisha kwa namna mbalimbali wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha mbogamboga. 

Hayo yameelezwa jana na Mhandisi wa kanda ya Mbeya wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Elibariki Mwendo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea skimu hiyo.

Mhandisi Mwendo alisema kuwa, Serikali imetumia kiasi cha shilingi Milioni mia mbili hamsini (250Milioni) kukarabati miundombinu ya skimu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa banio kubwa linalotoa maji katika chanzo cha maji cha mto Mbarali na mifereji inayopeleka maji mashambani.

“katika skimu hii wakulima wanajikita zaidi katika kilimo cha mbogamboga kama vile vitunguu, nyanya, matango, na hata zao la mpunga, ambapo kabla ya marekebisho na maboresho ya miundombinu hii, hali haikuwa nzuri kwani wakulima walikuwa wanajichotea maji kiholela ili kuweza kumwagilia mazao yao, lakini kwa sasa kama mnavyoona, maji yanakwenda moja kwa moja mashambani kwa utaratibu maalum ulivyopangwa ambapo kila mkulima ana zamu yake ya kuingiza maji mashambani tayari kwa kilimo, jambo ambalo limepelekea wakulima hawa kuongeza uzalishaji katika mazao wanayolima na kujiongeza pato la familia.” Alisisitiza Mhandisi Mwendo.

Mmoja wa wakulima wanaojishughulisha na zao la kilimo cha vitunguu katika skimu hiyo Bw. Yohana Mbuna (52) amesema amekuwa akijishughulisha na kilimo katika skimu hiyo kwa takribani miaka ishirini sasa, “ Kabla ya maboresho katika skimu hii hali ilikuwa mbaya kwanza tulikuwa tunalima bila kufuata utaratibu, tulikuwa tunagombania maji na hata mavuno hayakuwa mengi kwa heka moja nilikuwa napata magunia 30 lakini kwa sasa kwa heka moja ninaweza kupata zaidi ya magunia 100 na hii hunisaidia kupata fedha za kusomesa watoto wangu, na ninalima vitunguu kama zao la biashara, pamoja na hilo mazao mengine ya chakula kama mpunga ninalima kwa ajili ya familia yangu.” Alisema Bw. Mbuna.


Katika Picha Mhandisi Elibariki Mwendo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji akizungumza kuhusu maboresho yaliyofanywa katika banio (halipo pichani) lililopo katika chanzo cha maji cha mto Mbarali kinachopeleka maji katika skimu ya umwagiliaji ya Igomelo, nyuma pichani ni mto Mbarali.
Bibi Victoria Kinyega akifanya kazi ya kuchambua vitunguu katika skimu ya umwagiliaji wa Igomelo.
Vijana wanaofanya kazi katika shamba la vitunguu kwenye skimu ya Igomelo iliyopo Mbarali Mkoani Mbeya wakijaza vitunguu katika gunia maarufu kwa jina la net, tayari kwenda sokoni kuuzwa.
Kulia Afisa Kilimo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kanda ya Mbeya, Bw. Mnadi Taribo akimuelezea mgeni aliyetembelea shamba la mpunga katika skimu ya Umwagiliaji Igomelo, kuhusu teknolojia ya kisasa ya kilimo cha mpunga inayotumia kiasi kidogo cha maji, yaani kilimo shadidi.
moja ya ghala la kuifadhia vitunguu linalotumiwa na wakulima katika skimu ya umwagiliaji ya Igomelo.
Miundombinu inayopeleka maji katika mashamba ya mazao ya mbogamboga na mpunga katika skimu ya umwagiliaji ya Igomelo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...