Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza na waandishi
wa habari, kuelezea mipango na mikakati ya Benki hiyo katika mkutano
uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam, Oktoba 10,
2018.
Mkurugenzi
Mtendaji Mpya wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Mussa Nsekela
amewahakikishia Wateja, Wanahisa na Wadau wote wa Benki ya CRDB kuwa
Benki hiyo ipo kwenye mikono salama na itaendelea kukua pamoja na
kuzalisha faida kama ilivyotarajiwa. Bwana Nsekela aliyasema hayo katika
Mkutano na Waandishi wa habari wenye lengo la kumtambulisha rasmi
uliofanyika katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam.
Akielezea
kuhusu vipaumbele vyake, Ndugu Abdulmajid Mussa Nsekela alisema kuwa
kwa kushirikiana na viongozi na wafanyakazi wa Benki hiyo, amedhamiria
kufanya maboresho makubwa katika utoaji huduma kwa wateja kwa kutilia
mkazo katika maeneo matano muhimu, ambayo ni uboreshaji wa mifumo na
taratibu za utoaji huduma, ili ziendane na mahitaji halisi ya wateja na
soko, kuongeza weledi na umahiri wa wafanyakazi, kuwekeza kwenye
teknolojia ya kisasa, kukuza biashara katika nyanja zote ili kuendana na
kasi ya serekali ya awamu ya tano. Atahakikisha Benki inafanya vizuri
na kupata faida zaidi ili kutoa gawiwo nono kwa wanahisa. “Tutakuwa
tukiboresha mara kwa mara taratibu za jinsi ya kupata na kutumia huduma
zetu. Tunataka upatikanaji na utumiaji wa huduma za Benki CRDB uwe
rahisi, huku tukiendelea kusizogeza huduma hizo karibu zaidi na wateja
wetu” alisema Ndugu Nsekela.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay akitoa hotuba yake
kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid
Nsekela, kuzungumza na waandishi wa habari, katika mkutano uliofanyika
kwenye hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam, Oktoba 10, 2018.
Akifafanua
zaidi juu ya uboreshwaji wa huduma na mikakati ya Benki ya CRDB katika
eneo hilo muhimu, Ndugu Nsekela alisema kwa kipindi kifupi kijacho
Benki ya CRDB itajikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidigitali
(innovative products and services) itakayowezesha kuwafikia wateja
wengi zaidi, kwa urahisi zaidi, mahali popote walipo na hivyo
kuwaondolea wateja wao ulazima wa kutembelea matawi ya Benki ya CRDB
pindi wanapohitaji huduma. “Tutatumia fursa ya kuwa zaidi ya watanzania
milioni 19.3 wanatumia simu za mikononi kufanya miamala yao na
kuwashawishi kutumia bidhaa zetu za SimBanking na SIMAccount ambazo
nazo hutoa huduma kama hizo” alisema.
Akiongelea
kuhusu mikakati ya kusogeza huduma kwa wateja, Ndugu Nsekela alisema
Benki ya CRDB imejiwekea malengo ya kufikisha huduma katika wilaya zote
nchini ifikapo mwaka 2022. Na wamejiwekea lengo la kuongeza Mawakala
wake wa FahariHuduma katika kila kona ya nchi. Ndugu Nsekela alisema pia
Benki hiyo pia ina mpango wa kuendelea kupanua wigo wa huduma zake nje
ya nchi.
Mkurugenzi
wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Tully Esther
Mwambapa akizungumza jambo wakati akiongoza mkutano baida ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela na waandishi wa habari,
uliofanyika kwenye hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam, Oktoba 10,
2018.
Akielezea
kuhusu mahusiano baina ya Benki hiyo na Serikali na wadau wengine,
Ndugu Nsekela alisema kuwa Benki ya CRDB inaitambua Serikali kama
Mwanahisha wake na mdau mkubwa wa biashara. “Benki ya CRDB itaendela
kuthamini mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na Serikali na taasisi
zake na tutaendelea kubuni huduma na bidhaa mbalimbali mahususi kwa
ajili ya kufikia mahitaji ya Serikali pamoja na wafanyakazi wake mmoja
mmoja.
Tunajivunia
kuwa mmoja wa wadau wakubwa wa Serikali ili kwa pamoja tuweze kujenga
uchumi wa nchi hususani katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika
kujenga uchumi wa kati wa Viwanda,” alisisitiza Ndugu Nsekela.
Ndugu
Nsekela alimalizia kwa kusema hali ya uchumi nchini inatoa fursa kubwa
ya ukuaji kwa mabenki nchini huku akibainisha kuwa Benki ya CRDB
itaendelea kutia mkazo katika kuhudumia wateja Wakubwa, Wadogo na wa
Kati pamoja na Biashara ya kilimo pamoja na kuwawezesha wawekezaji
kwenye sekta ya viwanda ili kujenga Tanzania ya viwanda.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay akijadiliana jambo
na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela wakati wa
mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika kwenye hoteli ya Serena,
Jijini Dar es salaam, Oktoba 10, 2018.
Akizungumza
katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB
Ndugu Ally Laay alisema Bodi hiyo ina amini kuwa Ndugu Nsekela ni mtu
sahihi kabisa wa kuongoza Benki ya CRDB na kuahidi kumpa ushirikiano wa
kutosha.
Ndugu
Laay pia alitumia nafasi hiyo kumshukuru Dkt. Kimei kwa mchango wake
kwa Benki ya CRDB kwa kipindi cha miaka 20 aliyoiongoza. “Ni kazi ngumu
sana, lakini Dokta Kimei ameifanya kwa kujitoa na weledi wa hali ya juu
sana,” alisema Ndugu Laay.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Ally Laay akisalimiana na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela pamoja na Naibu
Wakurugenzi wa Benki hiyo Dorah Ngariga wa Huduma Shirikishi (wa pili
kulia) na Kushoto ni Esther Kitoka anayesimamia Uendeshaji na Huduma kwa
Wateja, wakati wa mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika kwenye
hoteli ya Serena, Jijini Dar es salaam, Oktoba 10, 2018.
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...