Wataalam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) waliokuwa wakitoa huduma ya matibabu kwa njia ya mkoba kwa kushirikiana na watalaam wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma mkoani Mara wameitimisha huduma hiyo leo Ijumaa baada ya kuwaona wagonjwa zaidi 1960 na kuwafanyia upasuaji zaidi wagonjwa 146.
Awali wataalam wa Muhimbili walikuwa watoe huduma ya matibabu kwa wananchi wa Mkoa wa Mara pamoja na kuwajengea uwezo watalaam wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma kwa muda wa wiki moja, lakini uongozi wa Muhimbili ulilazimika kuongeza siku saba kutokana na wingi wa wagonjwa walijitokeza kutoka Mkoa wa Simiyu, Mwanza na Shinyanga kwa ajili ya kupata huduma za kibingwa.
Wakati akihitimisha huduma hiyo leo  Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Joachim Eyembe aliwashukuru wataalam wa Muhimbili kwa kutoa huduma za kibingwa kwa kushirikiana na wataalam wake.
“Tunawapongeza sana kwa mara nyingine kwa ujio wenu, na tutawasiliana na uongozi wa Muhimbili ili tuwaombe mrudi tena Musoma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Mara. Siwezi kueleza furaha yangu kwa ujio wenu kwani naamini wataalam wangu wamejifunza mengi kutoka kwenu na wananchi wamepata huduma za kibingwahi,” amesema Dkt. Eyembe.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Nje, Dkt. Farbian Besiyegwa wa hospitali hiyo amesema amejifunza mambo mengi kutoka kwa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Dkt. Brighton Mushengezi wa Muhimbili.
“Kwa kweli nashukuru kufanya kazi na Dkt. Brighton, amenifundisha mambo mengi, hivi sasa  natamani kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya ndani,” amesema Dkt. Besiyegwa wakati wa kuwaaga wataalam wa Muhimbili.
Akizungumzia changamoto ambazo zimebainishwa na watalaam wa Muhimbili, Dkt. Eyembe kwa niaba ya uongozi wa hospitali hiyo ameahidi kushughulikia changamoto zote ili kuboresha zaidi huduma za afya katika hospitali hiyo.
Mganga mfawidhi ameahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kuwapatia mafunzo zaidi wataalam wake pamoja na kuboresha maeneo ya kutolea huduma ili kufikia malengo ya hospitali hiyo ya kuwa moja hospitali kubwa ya rufaa inayotoa huduma bora nchini.
Naye daktari Bingwa wa Macho wa Muhimbili, Dkt. Neema Kanyaro amesema wataalam wenzake walipewa ushirikiano mkubwa na wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma.
 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Musoma mkoani Mara, Dkt. Joachim Eyembe leo akiwaaga wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kumaliza kutoa huduma ya matibabu kwa njia mkoba kwa kushirikiana na wataalamu wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma.
 Baadhi ya wataalamu wa Muhimbili wakiwa kwenye kikao cha kuagana leo na wataalam wa Hospitali ya Rufaa ya Musoma katika ofisi za Mganga Mfawidhi.
 Baadhi ya wataalam wa Hospitali ya Rufaa Musoma wakiwa kwenye kikao hicho leo.
Wataalam wengine wa Hospitali ya Rufaa Musoma wakifuatilia kikao hicho leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...