ABIRIA wawili Raia wa Sudan Kusini na Syria leo wamekamatwa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) wakisafirisha fedha taslim dola elfu 70 za Kimarekani sawa na shilingi milioni 156 za Kitanzania na paundi 3410 za Sudan bila kufuata taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la JNIA, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi, Barnabas Mwakalukwa alimtaja Raia wa Sudan Kusini Bi. Nada Zaelnoon Ahamed (38) mwenye hati ya kusafiria namba P01563534 amekamatwa saa 10:00 jioni akiwa eneo la ukaguzi wakati akiingia ndani tayari kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ 485) akielekea Nairobi.

Hata hivyo, Afande Mwakalukwa amesema abiria huyo mbali na fedha hizo za Kimarekani pia amekamatwa na paundi za Sudan 3410, ambazo zote kwa pamoja alishindwa kutoa taarifa ya fedha alizokutwa nazo kwa mujibu wa sheria ya utakatishaji fedha ya mwaka 2006 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Pia alimtaja Bw. Mohamed Belal (31), Raia wa Syria mwenye hati ya kusafiria namba 003-16L096876 aliyekuwa akisafiri kwa ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia (ET 864) kuelekea Syria kupitia Addis Ababa amekamatwa na dola za kimarekani 10,000 sawa na Tsh. milioni 20 za Kitanzania, ambazo naye alishindwa kuzitolea taarifa. “Watuhumiwa wote wawili wamezuiwa na hawawezi kuendelea na safari zao kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria zilizopo,” amesema Afande Mwakalukwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewapongeza maafisa usalama wa JNIA kwa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu pamoja na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha wasafiri, wadau na maeneo yote ya viwanja vya ndege yanabaki salama na vitendo vya kiuhalifu havina nafasi katika viwanja hivyo. Bw. Mayongela amesema pamoja na watumishi hao kufanya kazi katika wakati mgumu kutokana na baadhi ya abiria kuwa watata kila wanapotaka kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni.


Kamishna Msaidizi na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa akinyanyua juu moja ya bunda la Dola za Kimarekani zilizokamatwa leo kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), zikisafirisha isivyo halali na raia wa Sudan Kusini Bi. Nada Zaelnoon Ahamed na Bw. Mohamed Belal, raia wa Syria. 
Jumla ya Dola za Kimarekani 70,000 sawa na Tsh. milioni 156 za Kitanzania zikiwa zimekamatwa leo kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), zikisafirishwa na Raia wawili wa Syria Bw. Mohamed Belal na Bi. Nada Zaelnoo Ahamed raia wa Sudan Kusini kwa kutofuata taratibu. 
Bi.Nada Zaelnoon Ahamed (38) Raia wa Sudan Kusini (katikati mwenye ushungi) akiwa mbele ya waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), baada ya kukamatwa na dola 60,000 za Kimarekani na Paundi 3410 za Sudan. 

Raia wa Syria, Bw. Mohamed Belal (31) mwenye fulana nyeupe akiwa mbele ya waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), baada ya kukamatwa na dola 10,000 za Kimarekani, ambazo hakuzitolea taarifa kwa Maafisa wa Forodha wa kiwanjani hapo. 
Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Paul Rwegasha (kushoto) akimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa (aliyesimama) alipokuwa akitoa maelezo kwa waandishi wa habari leo ya kukamatwa kwa Raia wawili wa Sudan Kusini na Syria waliokuwa wakisafirikisha fedha taslim milioni 156 bila kufuata sharia. 
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wa pili kulia) akisisitiza jambo kwenye mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) uliofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Pili la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), wakati walipokamatwa Raia wawili wa Syria na Sudan Kusini wakisafirisha mamilioni ya fedha bila kufuata taratibu.

Kusoma zaidi BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...