Na Greyson Mwase, Songwe

Serikali kupitia Wizara ya Madini imepiga marufuku usafirishwaji wa kaboni kwa ajili ya kuchenjulia madini ya dhahabu kutoka mkoa mmoja hadi mwingine na kusisitiza kuwa haitasita kumchukulia hatua za kisheria mchimbaji wa madini atakayekiuka agizo hilo.

Agizo hilo limetolewa leo tarehe 18 Oktoba, 2018 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo katika mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Saza kilichopo wilayani Songwe mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremeah, Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko, Maafisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi na Mhandisi Godfrey Nyanda, vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya pamoja na waandishi wa habari.

Akizungumza na wachimbaji hao, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Madini kupiga marufuku usafirishwaji wa kaboni kutoka katika mkoa mmoja kwenda mwingine tangu Juni mosi mwaka huu lilikuwa ni kuhakikisha kila mkoa unapata mapato stahiki kupitia ujenzi wa mitambo ya kuchenjua madini kwa kutumia kaboni.

“Kama Serikali tunataka kuhakikisha kila mkoa unajenga mitambo ya kuchenjua madini badala ya kwenda kuchenjulia katika mikoa ya jirani kwa kutumia kaboni na kukosa mapato stahiki,” alifafanua Nyongo. Alisisitiza kuwa, Serikali haitasita kutaifisha kaboni itakayokamatwa ikisafirishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ikiwa ni pamoja na kuwachukulia wahusika hatua za kisheria.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Saza kilichopo wilayani Songwe mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 18 Oktoba, 2018. 
Msimamizi wa uchimbaji madini katika Mgodi wa Dhahabu wa Sunshine uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe, Evarist Lukuba (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto mbele) mara alipofanya ziara katika mgodi huo. 
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa New Luika uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe, Honest Mrema (wa pili kulia mbele) akielezea majukumu ya mgodi huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo pamoja na msafara wake mara alipofanya ziara katika mgodi huo. 
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa New Luika uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...