Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii

TAMASHA la kihistoria la utalii linatarajiwa kufanyika visiwani Zanzibar kuanzia Oktoba 17 hadi 19 mwaka huu katika hoteli ya Verde, Mtoni visiwani humo na hiyo ni katika mpango kazi wa kupunguza umaskini na kuendeleza sekta ya utalii visiwani humo.

Akizungumza na vyombo vya habari Waziri wa Habari, utalii na mambo ya kale wa Zanzibar Mh. Mahmoud Kombo amesema kuwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein anatarajiwa kuzindua tamasha hilo akiambatana na viongozi wengine wa kitaifa akiwemo aliyekuwa Rais wa Zanzibar Dr. Amani Abeid Karume, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassani, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Waziri wa utalii na maliasili kutoka Tanzania bara Dkt. Hamis Kigwangalla.

Mahmod ameeleza kuwa tamasha hilo ni fursa na litawavutia wawekezaji, wamiliki wa hoteli na wamiliki wa kampuni za kitalii wazawa na wageni kwa kutangaza bidhaa zao za kitalii na amesema kuwa shughuli za kitalii zimechangia kwa asilimia kubwa sana katika ukuaji wa uchumi na hiyo ni kutokana na ubora wa huduma zitolewazo katika sekta hiyo.

Aidha amesema kuwa makampuni 150 na waoneshaji wa bidhaa za kitalii zaidi ya 130 kutoka ndani na nje ya nchi wanataraji kushiriki katika tamasha hilo na hiyo ni baada ya kutoa fursa kwa wadau hao kuja kujifunza na kupata semina za utalii wa ndani.

Kuhusiana na hali ya utalii visiwani humo Mahmoud ameeleza kuwa kwa mwaka 2017 zaidi ya watalii milioni moja waliingia nchini na watalii laki nne walitembelea Zanzibar na kwa mwaka huu wamevuka malengo kwa  kufikia watalii laki tano na hiyo ni kwa kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein.

Kuhusiana na mchango wa utalii katika uchumi wa taifa Mahmoud amesema kuwa asilimia 27 ya uchumi wa Zanzibar unachangiwa na shughuli za kitalii huku asilimia 80 ya uchumi wa hutokana na fedha za kigeni.

Pia ameeleza kuwa tamasha hilo litakuwa na maonesho, semina na kutolewa kwa tuzo takribani 21 kwa sekta za utalii zitakazotolewa Oktoba 20.

Mwisho amewataka wananchi wote wa bara na visiwani pamoja na wageni kutoka maeneo yote mbalimbali kuhudhuria tamasha hilo la aina yake na sio kwa utalii pekee bali kuona utamaduni, ukarimu na malikale zipatikanazo Zanzibar na kwa wawekezaji na wafanyabiashara watumie fursa hiyo katika kutangaza bidhaa zao.

Kwa upande wake Katibu wa kamisheni ya utalii Zanzibar Dkt. Abdallah Mohamed amesema kuwa tamasha hilo la  ni kwa wote katika kuonesha na kudumisha mila na tamaduni zetu.

Kuhusu usalama amesema kuwa hali ni shwari kabisa katika maeneo yote hasa bandari, viwanja vya ndege na fukwe zote hivyo wananchi na watalii wawe huru katika kufurahia tamasha hilo la kipekee.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...